BURUNGA, Burundi: TIMU ya Kombaini ya Wilaya Makamba mkoa Burunga nchini Burundi imeibuka kuwa mabingwa wa mashindano ya Ujirani Mwema kwa mwaka 2025 baada ya kuifunga kombaini ya Wilaya Kigoma kwa penalti 4-2.

Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Nkurunzinza Peace Park Complex Mkoa Burunga nchini Burundi, timu hizo zilimaliza dakika 90 zikiwa hazijafungana.

Penalti za Makamba zilifungwa na Ndayikengerukie Raymond, Ntakirutimana Fernand, Irakoze Emanuel na Nkurunzinza Pierre, wakati yale ya Kigoma yalifungwa na Baraka Charles na Kassim Daud, ambapo pambano hilo lilichezeshwa na Mwamuzi Emanuel Sonda wa Tanzania na waamuzi wasaidizi walitoka Burundi.

Mabingwa hao wamezawadiwa kombe na faranga milioni saba sawa na Sh milioni 2.5 za Tanzania, wakati mshindi wa pili alizawadiwa Faranga milioni tano sawa na Sh milioni mbili za Tanzania.

Mashindano hayo ambayo mwaka huu  yamefanyika kwa mara ya tisa mfululizo yalishirikisha jumla ya timu nane, ambapo timu nne zilitoka Mkoa Kigoma Tanzania na timu nne zilitoka mikoa ya Burundi.

Fainali hiyo ilihudhuriwa na Mkuu wa mkoa Kigoma, Balozi Simon Sirro, Mwenyeji wa mashindano hayo Mkuu wa Burunga, Partfait Mboninyibuka, Mkuu wa Mkoa Muhunga nchini Burundi, Denise Ndaruhekere na viongozi mbalimbali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *