TANGA: Bodi ya Ushauri ya Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imeridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Pangani lililopo mkoani Tanga.

Bodi hiyo imeeleza mradi huo unaendelea vizuri na unatekelezwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya ‘scaffolding system installation’ inayoongeza ufanisi na ubora wa ujenzi wa madaraja makubwa.

Akizungumza wakati wa ziara ya bodi hiyo kukagua mradi huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TANROADS, Mhandisi Amin Mcharo, amesema bodi imefurahishwa na kasi ya utekelezaji wa kazi pamoja na matumizi ya teknolojia ya hali ya juu katika kusogeza na kujenga daraja hilo.

Ameongeza kuwa teknolojia ya hiyo inayotumika katika ujenzi wa Daraja la Pangani ni mfano wa ubunifu unaopaswa kuigwa katika miradi mingine ya barabara na madaraja inayotekelezwa nchini.

Amesisitiza kuwa bodi inatarajia mradi huo kukamilika kwa wakati kama ilivyopangwa.
“Tumeshuhudia kazi ikiendelea vizuri kwa kutumia teknolojia mpya ya scaffolding. Bodi imeridhishwa na hatua zilizofikiwa na tunatarajia mradi huu utakamilika kwa wakati,” alisema Mhandisi Mcharo.

Ameendelea kwa kusema kuwa, bodi inatamani miradi yote ya TANROADS nchini itekelezwe kwa kasi na ubora unaoonekana katika mradi wa Daraja la Pangani.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwahusisha wataalam wa ndani ili kujenga uwezo wao kitaalamu kupitia kujifunza teknolojia mpya zinazotumika katika miradi mikubwa ya kimkakati.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta, amesema ujenzi wa Daraja la Pangani umefikia asilimia 70 huku akifafanua kuwa daraja hilo lina urefu wa mita 525 na linajengwa kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu inayolenga kuhakikisha uimara na usalama wa miundombinu hiyo kwa muda mrefu.

Mhandisi Besta ameongeza kuwa, daraja hilo litakapokamilika litaunganisha miji ya Bagamoyo na Dar es Salaam kwa upande mmoja, na kuunganisha mkoa wa Tanga na mpaka wa Horohoro kuelekea Mombasa kwa upande mwingine.

Vilevile amebainisha kuwa daraja hilo ni sehemu ya mradi wa barabara unaotekelezwa chini ya Mpango wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) unaounganisha Bagamoyo na Lungalunga.
Mtendaji Mkuu huyu wa TANROADS ameongeza kuwa, utekelezaji wa mradi huo utachochea shughuli za kiuchumi katika ukanda wa pwani kuanzia Tanzania hadi Kenya, hususan katika biashara, usafirishaji na uwekezaji.

Naye Mkurugenzi wa Miradi wa TANROADS, Mhandisi Japherson Nnko, amesema kwa sasa wakala huo una miradi zaidi ya 90 inayoendelea kote nchini, mikubwa na midogo ambapo pia amesema kati ya miradi hiyo, asilimia 55 inafadhiliwa na Serikali na asilimia 45 inafadhiliwa na mashirika ya maendeleo.

Mhandisi Nnko ameongeza kwa kusema kuwa, mradi wa Daraja la Pangani unaendelea vizuri, huku changamoto nyingi za kitaalamu zikiwa tayari zimetatuliwa.
Vilevile ameeleza kuwa TANROADS inatarajia mradi huo kukamilika kwa wakati pamoja na barabara zake za maingilio ili magari yaanze kupita mara baada ya kukamilika.

Kwa mujibu wa mkandarasi, ujenzi wa Daraja la Pangani ulianza rasmi tarehe 07 Desemba, 2022 na umepangwa kukamilika Februari 05, 2027, hata hivyo, mkandarasi ameonesha matarajio ya kuukamilisha mradi huo mapema mwezi Oktoba, 2026.
Ujenzi wa Daraja la Pangani kwa kutumia teknolojia ya scaffolding unaonesha mwelekeo mpya wa TANROADS katika kutumia teknolojia za kisasa, sambamba na kuhakikisha uhamishaji wa maarifa na ujuzi kwa wataalam wa ndani kwa ajili ya maendeleo endelevu ya miundombinu ya barabara nchini.