BEKI wa kati wa Coastal Union, Christopher Oruchum amesema kikosi chao kwa sasa kimeimarika na kinacheza soka la kuvutia, tofauti na hali ilivyokuwa awali kabla ya ujio wa benchi jipya la ufundi chini ya kocha Mohamed Muya.

Muya aliyejiunga na Coastal Oktoba 6 mwaka huu akirithi mikoba ya Ali Mohamed Ameir, ameiongoza timu hiyo katika mechi tano za ligi na kushinda moja, sare tatu na kupoteza moja.

Coastal inashika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi hiyo, ikivuna alama tisa katika mechi nane, huku ikishinda mbili, sare tatu, na kupoteza tatu, ambapo imefunga mabao matano na kuruhusu sita.

Oruchum, raia wa Kenya, alijiunga na Coastal dirisha kubwa la msimu huu akitokea Pamba Jiji ya Mwanza, ambapo amekuwa hana uhakika wa namba kwani chini ya Muya hajaanza mechi yoyote.

Akizungumza na Mwanaspoti, Oruchum amesema chini ya Muya timu yao inaboreka kwa kulinda, kukaba na kushambulia vizuri, ikipoteza mechi moja tu dhidi ya Yanga tena kwa bao 1-0.

“Kwangu nawapa heko walimu kocha Muya na benchi lake la ufundi.”

 “Baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo kwa kuruhusu mabao manne jumla, sasa hivi tunajilinda vizuri sana na pia ukiangalia tunacheza mpira mzuri,” amesema Oruchum na kuongeza;

“Natarajia kwa muda tutakaoupata kabla ya Ligi kuanza Januari tutazidi kuimarika zaidi. Kwanza, mwendelezo wa mazoezi kama ilivyo kawaida tukiwa na timu na pia kutilia mkazo sana upungufu binafsi.”

Amesema atatumia muda uliopo wa mapumziko kujinoa ili kuimarika na kulishawishi benchi la ufundi kumpa namba kikosini.

“Hadi sasa timu imekuwa ikiongezeka ubora mechi baada ya mechi. Tulianza vizuri tukapoteza mechi mbili ila baada ya hapo walimu nawashukuru kwa kugundua tatizo letu na hivi sasa nadhani tukirudi baaada ya mapumziko tutakuwa bora zaidi,” amesema.

Akizungumzia ushindani katika Ligi Kuu Bara, amesema; “Kila siku inakua ngumu kutokana na ushindani mkubwa na uwekezaji mkubwa uliopo. Kwangu kucheza katika ligi namba nne Afrika ni faraja kubwa, kwani ni kitu kizuri katika kukuza na kujenga kipaji changu.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *