TUME ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliyotokea Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 ikitegemewa na wadau mbalimbali kuimarisha umoja baada ya kuhitimisha utekelezaji wa majukumu yake.

Watu wa kada tofauti waliozungumza na HabariLEO, wamesema wana imani ripoti watakayoitoa itakidhi haja ya Watanzania na kuwezesha taifa kuendelea kuwa na umoja. Miongoni mwa wazungumzaji, wameeleza kuguswa na mbinu ya uchunguzi jumuishi wa wananchi wote wakisema inasaidia kukusanya ushahidi mpana na wa kina unaowezesha tume kupata taswira kamili ya tukio.

Katika taarifa yake, tume imewaalika wananchi wote, asasi za kiraia, viongozi wa dini, vyama vya siasa, makundi ya vijana, na wadau wengine wote kutoa taarifa, ushahidi, maoni, na mapendekezo yatakayoisaidia katika uchunguzi. SOMA: Mbowe ataja faida maridhiano na serikali

Tume imesisitiza kuwa itahifadhi usiri kwa watoa taarifa ambao hawatapenda kujulikana na wengine huku ikisema mafanikio yake yatategemea ushirikiano wa kila mwenye taarifa inayoweza kusaidia kujua ukweli. Tume ya uwazi, shirikishi Wachambuzi wana mtazamo chanya juu ya utekelezaji wa majukumu wa tume wa kuita kila mwenye taarifa kuziwasilisha wakisema hatua hiyo inadhihirisha uwazi, ushirikishwaji na haki katika kufikia ukweli.

Hatua hiyo inatajwa kuwa ni ishara ya dhamira ya kweli ya kufikia uelewa mpana wa kilichotokea. “Tume inapotoa nafasi kwa kila aliye tayari kuwasilisha taarifa, inaondoa dhana ya upendeleo na kujenga mazingira ya kuaminika kwa matokeo yatakayopatikana,” alisema mchambuzi, mshauri wa masuala ya habari, siasa na biashara, Dereck Murusuri. “Tume kutaka kila mwenye lolote analojua kuhusu yaliyotokea aende akutane nayo hiyo pekee yake ni digrii kubwa sana ya uwazi ikionesha ambavyo tume imedhamiria kutenda haki.

Dk Samia na serikali yake wameishangaza dunia mpaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekubaliana na njia aliyochukua na kupongeza kuwa ni namna ya kutafuta ukweli ili kutibu tatizo,” alisema Murusuri. Wachambuzi hao wameeleza kwamba kitaalamu, mbinu ya uchunguzi jumuishi ina faida kadhaa muhimu ikiwamo kusaidia kukusanya ushahidi mpana na wa kina unaowezesha tume kupata taswira kamili ya tukio.

Mbinu hiyo inatajwa kuwa inaongeza uwajibikaji wa taasisi na watu binafsi, kwani kila upande unatambua kuwa sauti yake inasikika na mchango wake unaweza kuathiri mwelekeo wa mapendekezo ya mwisho. Njia hiyo inatajwa pia kwamba inajenga imani ya umma hususani katika mazingira ambayo wapo baadhi ya watu wenye mashaka na wakosoaji kwa misingi ya itikadi za siasa.

Kusikilizwa kwa watu wote bila kuegemea viongozi pekee, kunatajwa kuwa kunaiweka tume katika mazingira ya kuaminika pale itakapotoa mapendekezo yake. “Hata kama si kila mtu ataridhika na hitimisho, angalau kuna uhakika kwamba kila aliyekuwa na cha kusema alipata nafasi,” anasema kiongozi mmoja wa asasi ya kiraia.

Tuipe nafasi Tume Mchambuzi wa masuala ya siasa na uchumi ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda, alisema, “Tuipe nafasi tume ifanye kazi. Wajumbe hawa ni watu wenye weledi, taaluma na waandamizi, wanaweza kuja na ripoti nzuri tofauti na hisia hasi za baadhi ya watu”.

Kuhusu utaratibu wa kutoa maoni, alisema ni hatua nzuri na kushauri elimu zaidi itolewe kwa wananchi ili wajenge imani ya kutoa maoni yao kwa uhuru na kuondoa hofu ya kukamatwa. Dk Mbunda alisema umuhimu wa uchunguzi huo unaweza kuleta upatanisho na umoja wa kitaifa, kwani mashuhuda wanaweza kujitokeza kueleza madhila yaliyowakumba wapendwa wao, na kitendo cha kusimulia mbele ya tume hiyo kinaweza kuondoa uchungu.

“Mtu akienda kutoa ushuhuda, mfano mke aliyeshuhudia mume wake akipigwa risasi na kufariki, anatoa ule uchungu na wakati mwingine atalia. Kitendo hicho kinaondoa yale yanayomuumiza moyoni na ni rahisi kuleta upatanisho na suluhu,” alisema Dk. Mbunda.

Ushirikishaji vijana Mchambuzi wa siasa, Hamduni Marcel alisema si lazima vijana wawe sehemu ya wajumbe kwenye tume hiyo bali ni muhimu wakishirikishwa katika upatikanaji wa taarifa kwa kuielekeza tume na kutoa ushahidi unaohitajika.

Mchambuzi wa siasa, Dk Albanie Marcossy amesema tume hiyo itasaidia nchi kujipatia taarifa za ndani za kutumika na serikali na wadau wa dola kwa kubainisha kilichotokea kutoka kwa watu wanaowaamini na si kwa kutegemea taarifa za vyombo vya nje. “Hii tume inaanzisha hatua ya kuelekea mjadala wa wazi na shirikishi wa kutafuta suluhu ya mambo yaliyofanya tukafikia pale Oktoba 29.

Itategemea na uwezo, ukubwa na ukweli pamoja na kujituma kwa tume na wajumbe wake kama watakusanya taarifa za kutosha watachambua na kuandika ripoti na mapendekezo sahihi, hapo itatoa picha kama mambo waliyoyagundua yataisaidia nchi kusonga mbele kiasi gani,” alisema.

Marcossy amesema  uwepo wa tume hiyo ni ishara kwamba serikali imekubali kuwa kuna tatizo na ipo tayari kuchukua hatua kulitatua. Tume kutibu nchi Mwenyekiti wa Chama cha ADA – TADEA, Juma Ali Khatibu alisema uamuzi wa Rais Samia kufanya uchunguzi ni jambo jema kwa sababu pamoja na maridhiano lakini pia nia ni kujua chanzo cha tatizo ili kujua namna ya kulitibu. Rais Samia Suluhu Hassan aliunda tume hiyo Novemba 18, mwaka huu ikiongozwa na Mwenyekiti Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman.

Wajumbe wengine ni Jaji Mkuu mstaafu wa Mahakama ya Tanzania, Profesa Ibrahim Juma na Mwanadiplomasia na Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue. Pia, wamo Mwanadiplomasia na Balozi mstaafu, Balozi Radhia Msuya, Mwanadiplomasia na Balozi mstaafu, Paul Meela na Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) mstaafu, Said Mwema.

Wengine ni Mwanadiplomasia na Balozi mstaafu, Balozi David Kapya na aliyewahi kuwa Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Dk Stergomena Tax. Tume hiyo inatarajiwa kumaliza uchunguzi wake ndani ya siku 90

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *