
Dar es Salaam. Katika miaka ya hivi karibuni, dunia imegeukia kwa kasi kuhifadhi dhahabu kama njia salama ya kulinda thamani ya mali wakati wa misukosuko ya kiuchumi na kijiografia.
Benki kuu za nchi mbalimbali zimeongeza akiba ya dhahabu ili kupunguza utegemezi wa sarafu za kigeni na kuimarisha uthabiti wa mifumo ya kifedha.
Mvutano wa kisiasa, mabadiliko ya sera za fedha na hatari za mdororo wa uchumi vimeifanya dhahabu kuwa kimbilio salama kwa wawekezaji, hali ambayo imechochea kukua kwa mahitaji yake huku bei ya dhahabu ikiendelea kupaa.
Hali hii inaashiria kuwapo kwa imani kubwa ya wawekezaji kwa dhahabu kama hifadhi ya thamani ya muda mrefu na kinga dhidi ya mfumuko wa bei.
Kutokana na hali hiyo, bei ya dhahabu katika soko la dunia siku ya Jumatatu, Desemba 22, mwaka huu ilikuwa takribani karibu dola 4,410 za Marekani (Sh10.900 milioni) kwa wakia, ikifikia viwango vya juu kabisa katika historia kwa kuvuka dola 4,400 za Marekani (Sh10.87).
Kwa mujibu wa tovuti ya goldprice.org, bei ya dhahabu imepanda kwa asilimia 5 hadi 8 katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, sawa na ongezeko la dola 300 hadi 336 kwa wakia.
Ongezeko hilo limechochewa na mahitaji makubwa ya wawekezaji, ununuzi wa mali salama, matarajio ya kupunguzwa kwa viwango vya riba nchini Marekani, hali ya sintofahamu ya kijiografia, pamoja na kudhoofika kwa dola ya Marekani.
Akizungumza Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba anasema dhahabu ina nafasi ya kipekee kwa kuwa ina jukumu la pande mbili, mosi kama bidhaa ya biashara na kama chombo cha kifedha kinachoimarisha uchumi wa nchi.
“Kuongezeka kwa mauzo ya dhahabu nje ya nchi huingiza fedha za kigeni, jambo linaloweza kuboresha mizania ya akaunti ya sasa,” anasema.
Gavana Tutuba anasema kwa wachimbaji wa dhahabu, kupanda kwa bei kunamaanisha faida kubwa zaidi.
“Kwa gharama za uzalishaji zinazokadiriwa kuwa kati ya dola 1,000 hadi 2,000 kwa wakia, kampuni zinazouza kwa bei hizi za juu hupata faida kubwa, mtiririko mzuri wa fedha taslimu na uwezo wa kuwekeza upya, kulipa madeni na kupanua shughuli zao. Wanahisa pia hunufaika kupitia gawio kubwa zaidi, hivyo kufanya hisa za kampuni za madini kuvutia zaidi,” anasema.
Anabainisha kuwa kampuni kubwa kama Barrick Gold na AngloGold Ashanti ziko katika nafasi nzuri zaidi ya kunufaika kwani gharama nyingi za kudumu tayari zimeshalipwa, hivyo ongezeko la bei huingia moja kwa moja kwenye faida.
Gavana Tutuba anasisitiza kuwa dhahabu ni rasilimali ya kimkakati ya kiuchumi kwa Tanzania, kwani inaongeza mauzo ya nje, inaboresha mizania ya malipo na kuunga mkono uthabiti wa jumla wa uchumi.
Gavana anasema hayo wakati ambao ripoti ya tathmini ya hali ya uchumi ya mwezi Novemba mwaka huu inaonyesha kuwa mahitaji ya dhahabu yalipanda na kufikia kiwango cha juu zaidi, yakichochewa na matarajio ya kupunguzwa kwa kiwango cha riba na Benki Kuu ya Marekani.
Hali hiyo ilifanya mauzo ya dhahabu kuongezeka kwa asilimia 38.9 hadi kufikia Sh11.33 trilioni katika mwaka ulioishia Oktoba mwaka huu kutoka Sh8.15 trilioni kipindi kama hicho mwaka uliotangulia, ikichangiwa zaidi na kuongezeka kwa bei ya dhahabu kwenye soko la dunia.
Ina maana gani
Akizungumzia suala hili, mchambuzi wa masuala ya fedha, Christopher Makombe anasema kwa sasa dhahabu ndiyo bidhaa inayoongoza kwa kuingizia Tanzania mapato ya mauzo ya nje, ambapo mapato yanazidi dola bilioni 4.3 mwaka 2025.
Kupanda kwa bei hadi karibu dola 4,500 kwa wakia kutaongeza zaidi thamani ya mauzo ya nje, na kuingiza dola zaidi katika uchumi.
Anasema mapato zaidi ya mauzo ya dhahabu nje ya nchi yataimarisha akiba ya fedha za kigeni, kusaidia malipo ya uagizaji wa bidhaa kutoka nje, na kuchangia uthabiti wa thamani ya shilingi ya Tanzania.
“Mapato makubwa ya dhahabu yataimarisha akaunti ya sasa ya Tanzania, kwani mapato hayo yatasaidia kufidia gharama za uagizaji, hivyo kupunguza utegemezi wa mikopo ya nje,” anasema.
Anaongeza kuwa bei ya juu ya dhahabu huongeza mapato ya serikali kupitia tozo za mrabaha, kodi na ushuru wa mauzo ya nje kutoka sekta ya madini.
Kwa mapato hayo zaidi, serikali inaweza kuwa na uwezo mkubwa wa kufadhili huduma za umma, miundombinu, afya na elimu, ingawa hilo litategemea sera pana za kifedha na namna mapato hayo yatakavyosimamiwa.
Alibainisha kuwa sekta ya madini tayari inachangia sehemu kubwa ya Pato la Taifa (GDP) la Tanzania takribani asilimia 10 hivyo ongezeko la bei ya dhahabu litaongeza thamani ya uzalishaji na linaweza kuchochea ukuaji wa uchumi, hasa kama uwekezaji katika madini utaongezeka siku zijazo.
Mtaalamu wa uchumi, Profesa Aurelia Kamuzora anasema kuongezeka kwa bei wakati mwingi huchochewa na ukuaji wa uchache wa vitu vinavyotakiwa dhidi ya usambazaji uliopo.
Hali hiyo inaonyesha kuwa sasa nchi nyingi zinakimbilia kununua dhahabu ili kwa sababu imeonekana kuwa njia sahihi ya kulinda uchumi wao.
“Kinachoonekana sasa ni mahitaji kukua zaidi kuliko usambazaji wakati ambao fedha za nchi nyingi zinashuka thamani kutokana na kupanda kwa gharama za vitu vya kawaida na mabadiliko yanayoendelea duniani,” anasema.
Anasema upandaji wa bei unaleta fursa mpya ya kupata fedha za kigeni kwa sababu kama nchi huchimba madini hivyo ni vyema kuitumia kikamilifu nafasi hiyo wakati nchi nyingi zinaendelea kuinunua dhahabu na kuitunza kwa ajili ya baadaye.
Anasema hii ni ishara kuwa Tanzania inahitaji kuweka dhahabu nyingi zaidi kama akiba huku akiweka bayana kama kungekuwa na fedha za kutosha basi Tanzania ingenunua dhahabu yake yote inayozalishwa na kuihifadhi.
“Tukihifadhi tunakuwa na uhakika hata ikitokea fedha yetu imeshuka thamani kwa sababu mbalimbali inasaidia uchumi wetu uwe imara kwa sababu hivi sasa kuna mambo mengi ikiwemo mabadiliko ya tabianchi ni moja ya jambo ambalo linaloathiri mnyororo wa thamani ya uzalishaji na yanaweza kuathiri pia fedha pia,” anasema.
Anasema mabadiliko haya yanapogusa mnyororo wa thamani husababisha mfumuko wa bei kwani huathiri maeneo mbalimbali ikiwamo kilimo kinachotegemewa katika kuzalisha malighafi za viwanda vya bidhaa mbalimbali.