
Wakazi wa mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, wameanza kupiga kura katika uchaguzi wa baraza la mitaa, tukio la kihistoria kwani ni mara ya kwanza baada ya zaidi ya miaka 50 wananchi kuchagua wawakilishi wao moja kwa moja. Hata hivyo, hatua hii imegubikwa na upinzani wa vyama vilivyokataa kushiriki.
Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa saa 12 alfajiri kwa saa ya Mogadishu (saa 3:00 GMT) siku ya Alhamisi, na mistari mirefu imeonekana mapema asubuhi huku Wasomali wakijipanga kushiriki katika kile Rais Hassan Sheikh Mohamud alikitaja kuwa “ukurasa mpya katika historia ya taifa.”
Takribani nusu milioni ya wapiga kura walisajiliwa kupiga kura. Abdishakur Abib Hayir, mjumbe wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa, amesema kuwa takribani wagombea 1,605 wanashindania viti 390 vya mabaraza ya wilaya jijini Mogadishu. Baada ya wajumbe wa baraza kuchaguliwa, wao ndio watakaomchagua meya wa jiji.
Maafisa wa polisi 10,000 wanalinda doria Mogadishu huku wakipekua magari na watembea kwa miguu
Usalama katika mji mkuu umeimarika mwaka huu, lakini serikali bado inapambana na kundi la kigaidi lenye uhusiano na al-Qaeda, al-Shabab, ambalo lilifanya shambulio kubwa mwezi Oktoba.
Mara ya mwisho Somalia ilifanya uchaguzi wa moja kwa moja ilikuwa mwaka 1969, miezi michache kabla ya mapinduzi ya kijeshi ya Oktoba mwaka huo yaliyowaondoa raia madarakani kwa zaidi ya miongo mitatu.
Baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kufuatia kuanguka kwa utawala wa kijeshi wa Mohamed Siad Barre mwaka 1991, taifa hilo lilikumbatia mfumo wa uchaguzi wa moja kwa moja wa koo mwaka 2004, ambapo wawakilishi wa koo huchagua wanasiasa, ambao nao humchagua rais. Mfumo huu umekuwa ukikosolewa sana na wagombea wa urais.
Rais wa sasa, Hassan Sheikh Mohamud, ambaye ameshinda mara mbili kupitia mfumo huo, alitangaza mwaka 2023 dhamira yake ya kuhamia mfumo wa kura ya moja kwa moja kwa ngazi ya mitaa, kitaifa na urais.
Uchaguzi huu unafanyika wakati Somalia ikikabiliwa na changamoto kubwa za kiusalama katika maeneo karibu na mji mkuu. Al-Shabab, kundi linalotaka kuipindua serikali, lilianzisha mashambulizi makubwa Februari 2025 yaliyobatilisha mafanikio ya kijeshi ya serikali.
Wiki hii, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeongeza muda wa jukumu la kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika kinachosaidiwa na UN, ingawa kinakabiliwa na upungufu mkubwa wa fedha unaoweza kuhatarisha ufanisi na mwendelezo wake.