Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran  ametuma salamu kwa Papa Leo wa XIV, kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, akimpongeza kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Nabii Isa (amani iwe juu yake) na kuwadia Mwaka Mpya wa 2026.

Katika ujumbe wake wa Alhamisi, rais wa Iran amesisitiza kuhusu sifa za kiroho za Nabii Isa hasa uhuru, uadilifu na huruma, ambazo pia zimetajwa katika Qur’ani Tukufu, akizieleza kuwa ni mifano ya milele kwa wanadamu wote.

Rais Pezeshkian alionya kuwa katika zama hizi ambapo nguvu za mataifa makubwa hutumika bila mipaka na kuisukuma dunia kuelekea migogoro na maangamizi, changamoto za binadamu haziwezi kutatuliwa ila kwa hekima ya pamoja, tafakuri, na hatua huru za viongozi wa mataifa pamoja na wanazuoni. Alionyesha matumaini kuwa juhudi hizo zinaweza kufungua njia ya amani, usalama na uhuru kwa mataifa yaliyodhulumiwa.

Rais alihitimisha kwa kumtakia Papa afya njema, ustawi kwa Wakrsito, na amani ya kudumu duniani kote.

Wakati huohuo, Waziri wa Mambo ya Nje Abbas Araghchi naye ametoa salamu za pongezi kwa Wakristo duniani kote kwa kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Nabii Isa (amani iwe juu yake).

Kupitia ukurasa wake wa X, aliandika: “Nawatakia wote duniani wanaosherehekea kuzaliwa kwa Nabii Isa (AS) Krismasi yenye usalama, afya, amani na furaha.”

Araghchi amebainisha matumiani yake kwamba sherehe ya kuzaliwa kwa Mtume wa Amani na Huruma zitakuwa ni zenye baraka.   

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *