
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Venezuela ameisifu Iran kwa misimamo yake thabiti ya kutetea mamlaka ya kujitawala Caracas.
Kulingana na Pars Today, Yvan Gil Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela amesema katika taarifa rasmi ambapo aliihutubu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kushukuru na kuthamini misimamo thabiti ya Tehran katika kutetea mamlaka ya kujitawala Venezuela na eneo la Karibi.
Akitoa salamu kwa niaba ya Rais wa Venezuela Nicolas Maduro, Yvan Gil alisisitiza kwamba, Venezuela inashukuru sana himaya na uuungaji mkono wa Iran katika suala hili. Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela aliongeza: “Caracas inathamini sana kujitolea kwa Iran kwa uthabiti wa biashara ya kimataifa, ambayo kwa sasa inatishiwa na vitendo vya uchokozi na haramu vya Marekani.”
Yvan Gil pia aliishukuru Iran kwa kutoa wito kwa nchi zote kuonyesha upinzani wao mkubwa kwa tishio au matumizi yoyote ya nguvu ambayo ni kinyume na mkataba wa Umoja wa Mataifa.
Hapo awali, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ililaani hatua za hivi karibuni za kijeshi za Marekani dhidi ya Venezuela, ikizitaja kuwa tishio kwa usalama na utulivu katika Karibi na Amerika Kusini. Iran pia ilitoa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kushughulikia haraka hali hatari inayosababishwa na hatua ya Marekani ya kuingilia kati kinyume cha sheria katika masuala ya ndani ya Venezuela, ambayo inatambuliwa kama taifa huru na mwanachama wa Umoja wa Mataifa.
Msimamo wa Iran katika kuunga mkono Venezuela dhidi ya vitisho vya Marekani umejikita katika kanuni za sera ya kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu, ambayo imejikita katika uhuru, kukabiliana na misimamo ya upande mmoja, na kutetea mamlaka ya kitaifa ya nchi. Mbali na masuala ya kisiasa na kisheria, usaidizi huu pia una athari za kijiografia na kiuchumi na umesababisha kuimarika kwa uhusiano wa Tehran na Caracas.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikichukua msimamo thabiti na wazi katika kuilinda Venezuela dhidi ya shinikizo na vitisho vya Marekani katika miaka ya hivi karibuni. Msimamo huu si wa muda mfupi bali ni sehemu ya sera kuu ya Iran katika kukabiliana na upendeleo wa Marekani na kutetea uhuru na mamlaka ya kujitawala nchi. Iran imezingatia mara kwa mara vitendo vya Washington dhidi ya Caracas kuwa ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na tishio kwa amani na usalama wa dunia.
Sababu za himaya na uungaji mkono huu zinaweza kuchunguzwa katika mihimili kadhaa.
Mosi, uzoefu wa pamoja wa vikwazo na mashinikizo ya Marekani. Iran na Venezuela zimekuwa chini ya vikwazo vya kiuchumi na kisiasa vya Washington kwa miaka mingi, na tajiriba hii ya pamoja imekurubisha mitazamo ya mataifa haya mawili. Kwa kulaani vitendo vya Marekani dhidi ya meli za mafuta na anga ya Venezuela, kimsingi Iran inasisitiza kanuni ya kukabiliana na sera za utumiaji mabavu.
Pili, kufungamana Iran na kanuni na sheria za kimataifa na Hati wa Umoja wa Mataifa. Tehran imetangaza mara chungu nzima kwamba mashambulizi ya Marekani dhidi ya meli za kibiashara au vitisho dhidi ya mamlaka ya kitaifa ya nchi ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa. Msimamo huu umetolewa si tu katika kuitetea Venezuela bali pia katika kulinda utaratibu wa kimataifa unaozingatia sheria. Iran inaamini kwamba, kupuuza vitendo hivyo vya upande mmoja kunaweza kusababisha kusambaratika kanunii na sheria za kimataifa.
Tatu, engo za kijiografia na kiuchumi za uhusiano wa Iran na Venezuela. Licha ya umbali wao wa kijiografia, nchi hizo mbili zina uhusiano wa karibu katika nyanja za nishati na ushirikiano wa kiuchumi. Uuzaji wa mafuta nje, ushirikiano wa viwanda, na ubadilishanaji wa teknolojia ni sehemu ya uhusiano huu. Uungaji mkono wa Iran kwa Venezuela dhidi ya vitisho vya Marekani, pamoja na upande wa kisiasa, pia unasaidia kudumisha na kupanua ushirikiano huu.
Ukweli wa mambo ni kuwa, msimamo thabiti wa Iran katika kuiunga mkono Venezuela unapaswa kutambuliwa kama sehemu ya mkakati mkuu wa Tehran katika kukabiliana na sera za kibabe za Washington. Mkakati huu unategemea kanuni kama vile kutetea uhuru wa nchi, kupinga vikwazo vya upande mmoja, na kujitahidi kuunda utaratibu wa haki zaidi katika mahusiano ya kimataifa. Kwa kusimama upande wa Venezuela, Iran si tu kwamba inaunga mkono mshirika wa kisiasa na kiuchumi bali pia inatuma ujumbe wazi kwa ulimwengu kwamba: Kukabiliana na ubabe na kutetea mamlaka ya kitaifa ni sehemu muhimu ya sera ya kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu.