KIKOSI cha Simba kinatarajiwa kuingia kambini kesho Jumapili mara baada ya kocha mkuu mpya, Steve Barker na wasaidizi wake watakapowasili, lakini kuna beki mmoja wa kushoto kutoka Sauzi anatajwa kuwa katika rada za klabu hiyo ili kuimarisha kikosi hicho kupitia dirisha dogo.

Simba inadaiwa tangu mapema msimu huu ilikuwa ikimpigia hesabu beki wa kushoto wa Mamelodi Sundowns, Fawaaz Basadien, lakini mkataba uliwabana japo inaelezwa kuwa imerudi kwa jamaa baada ya kumnasa kocha Msauzi aliyewahi kufanya kazi na beki huyo.

Inadaiwa kuwa, beki huyo hana furaha Mamelodi kutokana nna kukosa nafasi ya kucheza na kuna uwezekano Simba ikamnasa kwa mkopo, huku ikielezwa Naby Camara aliyechukuliwa kama beki wa kushoto kushindwa kutumika katika eneo hilo kuziba nafasi ya Valentin Nouma.

Simba kwa sasa inamtegemea zaidi Anthony Mligo aliyeziba nafasi ya Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, huku akiwa hana msaidizi wa uhakika kwa vile Naby anatumika zaidi kama kiungo, japo inaelezwa huenda akatemwa dirisha dogo kuruhusu Basaidien aingie kama dili litatiki.

Basadien anatajwa kuwa tayari kujiunga na wekundu wa Msimbazi ili kuungana tena na kocha wake wa zamani, Steve Barker, aliyewahi kufanya naye kazi kwa mafanikio akiwa Stellenbosch FC, licha ya kuhusishwa pia na Raja Casablanca ya Morocco.

SIMB 01

Mchezaji huyo alikuwa katika rada za Simba tangu msimu uliopita baada ya kuonyesha kiwango bora katika Kombe la Shirikisho Afrika akiwa na Stellenbosch chini ya Barker, lakini dili hilo halikufanikiwa na hatimaye akaamua kujiunga na Mamelodi Sundowns.

Hata hivyo, licha ya kuwa sehemu ya moja ya klabu kubwa Afrika, Basadien ameripotiwa kukosa furaha kutokana na nafasi ndogo ya kucheza chini ya kocha Miguel Cardoso.

Hadi sasa, beki huyo ametumika katika mechi tano tu za Ligi Kuu Afrika Kusini, akicheza jumla ya dakika 220, huku Mamelodi ikicheza jumla ya mechi 21 katika mashindano yote msimu huu, ikiwemo nne za Ligi ya Mabingwa Afrika.

Basadien alijiunga na Stellenbosch FC kabla ya msimu wa 2022/23 na kucheza mechi 111 katika mashindano yote kwa kipindi cha misimu mitatu, akithibitisha uwezo wake mkubwa akiwa nafasi ya beki wa kushoto.

Katika kipindi hicho, alifunga mabao manane na kutoa pasi 18 za mabao, mchango uliosaidia Stellenbosch kutwaa ubingwa wa Carling Knockout 2023, kumaliza nafasi tatu bora mfululizo katika Ligi Kuu ya Betway na kufika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Ubora huo ulimfanya kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Msimu wa klabu pamoja na Tuzo ya Wachezaji kwa Wachezaji msimu wa 2024/25, pia akiteuliwa kuwania tuzo ya Bao Bora la Msimu.

Kwa upande wa kimataifa, Basadien aliwahi kuichezea timu ya taifa ya Afrika Kusini, Bafana Bafana, akipata mechi tano za kimataifa na kuwa sehemu ya kikosi kilichosaidia taifa hilo kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2025.

Licha ya Simba kudaiwa kumpigia hesabu, lakini Raja Casablanca imeripotiwa kuwasilisha ofa rasmi kwa Mamelodi ikihitaji huduma ya beki huyo wa kushoto, huku kocha mkuu wa timu hiyo, Fadlu Davids ambaye awali alimpendekeza Simba kabla ya kuondoka, akiwataka mabosi wa klabu hiyo kufanya kila linalowezekana kukamilisha usajili huo dirisha dogo.

Hata hivyo, Raja wanakutana na ushindani mkali kutoka Simba ambao nao wameonyesha nia ya kumnasa mchezaji huyo, wakiamini anaweza kuimarisha upande wa beki ya kushoto ambayo imeonakana kupwaya.

SIMB 02

MSIKIE MWENYEWE

Basadien alitafutwa na Mwanaspoti jana na kusema alifurahi aliposikia kocha Barker anahamia Simba.

“Nilivyosikia amejiunga na Simba nilimtumia ujumbe na kumpongeza, tumekuwa na mahusiano mazuri kwa muda ambao tumefanya wote kazi. Kuhusu uwezekano wa kufanya tena kazi kwa mara nyingine ni kitu kinachowezekana lakini kwa sasa mimi ni mchezaji wa Mamelodi,” amesema beki huyo.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani kutoka Simba, klabu hiyo ipo tayari kumnasa beki huyo wa kushoto kwa mkopo wenye kipengele cha kumsajili jumla mwisho wa msimu kama ilivyofanya kwa Neo Maema mwanzoni mwa msimu huu, japo anasubiriwa kocha mpya kuja kuamua hatma ya usajili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *