MSIMU mpya wa michuano ya Kombe la Mapinduzi kwa mwaka 2026 inatarajiwa kuanza kesho Jumapili kwa klabu 10 ikiwamo Mlandege zitaanza mshikeshike wa wiki kama mbili kusaka taji hilo.

Mlandege kwa sasa ndio watetezi ikishikilia taji hilo kwa misimu miwili mfululuzo ya mwaka 2023 na 2024, ikiwa ni rekodi tangu michuano ya Kombe la Mapinduzi ilipoanza kushirikisha timu za nje ya Zanzibar kuanzia mwaka 2007 kwani kabla ya hapo, zilikuwa zikicheza zenyewe kutoka visiwani.

Mlandege imejijengea heshima hiyo kwa kuzifunga timu za Tanzania Bara na kubeba ubingwa ikianza mwaka 2023 dhidi ya Singida Big Stars ambayo sasa inatambulika kama Fountain Gate ikishinda 2-1, kisha mwaka 2024 ikaifunga Simba bao 1-0. Mechi zote zilichezwa Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Unguja.

Baada ya msimu wa 2025 michuano ya Kombe la Mapinduzi kuhusisha timu za taifa na kufanyika kisiwani Pemba, safari hii inarudi upande wa klabu na Mlandege inakwenda kufungua dimba dhidi ya Singida Black Stars.

MLAND 01

Mechi hiyo ufunguzi ikiwa imepangwa kuchezwa Unguja, fainali ya Kombe la Mapinduzi itafanyika Pemba kwenye Uwanja wa Gombani.

Mlandege inayoingia uwanjani ikiwa kama bingwa mtetezi kutokana na mara ya mwisho kufanyika Kombe la Mapinduzi kwa timu za klabu ilichukua ubingwa mfululizo, imejipanga kuendeleza ubora wake.

MIPANGO YA 2026

Katika mahojiano maalum kati ya Mwanaspoti na Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Sabri China, anasema wamejipanga vizuri kuhakikisha wanatetea taji hilo kwenye ardhi ya nyumbani.

“Kama kawaida yetu tumejipanga kufanya vizuri, tunataka kuona ule ubingwa tuliouchukua mwaka 2023 na 2024, tunauchukua tena safari hii ili kuzidi kuonyesha ubora wetu,” anasema.

MLAND 02

China anasema kwao kushiriki Kombe la Mapinduzi ni fursa kwa wachezaji wazawa kuonyesha uwezo wao ili kujitangaza na kununuliwa na klabu za nje ya Zanzibar.

Anasema kutokana na fursa hiyo, ndiyo sababu mojawapo inayoifanya Mlandege kuchezesha wazawa kwa lengo la kuwapa uzoefu wa mashindano makubwa ya aina hiyo kwani Ligi ya Zanzibar pekee haitoshi kuwajenga.

“Hivyo yanapotokea mashindano kama haya, inakuwa fursa kwa wachezaji wetu kupata vitu vipya vinavyowaongezea katika maisha yao ya kucheza mpira,” anabainisha.

KUNDI LA KIBABE

Katika makundi matatu ya Kombe la Mapinduzi 2026, lile la A pekee ndilo lina timu nne, huku mengine yakiwa na timu tatu.

Mlandege ipo kundi A na timu za Azam, Singida Black Stars za Tanzania Bara na URA kutoka Uganda.

Kupangwa na timu mbili za Tanzania Bara na moja ya nje ya nchi, kunaifanya Mlandege kuwa na mtihani mzito wa kufanya kuvuka hatua hiyo na kufuzu nusu fainali.

Mlandege ndiyo timu pekee ya Zanzibar itakayocheza dhidi ya wapinzani kutoka Tanzania Bara na nje ya mipaka ya Tanzania.

Hata hivyo, rekodi ya Mlandege katika misimu miwili iliyocheza Kombe la Mapinduzi ikizifunga timu za Tanzania Bara na kubeba ubingwa, huku pia 2023 ikiiondosha APR ya Rwanda hatua ya nusu fainali, inaipa jeuri ya kutomuogopa mpinzani yeyote.

MLAND 03

“Hatuna sababu ya kumuogopa mpinzani yeyote katika mashindano haya, wao wamejipanga na sisi tumejipanga kuhakikisha tunafanya vizuri,” anasema China. 

FAIDA ZA KUSHIRIKI

China anasema wamepata faida kubwa kupitia Kombe la Mapinduzi ikiwemo kutwaa ubingwa mara mbili mfululizo mbele ya klabu zinazoshiriki mashindano ya kimataifa.

Pia, anasema Mlandege imefanikiwa kuuza wachezaji kupitia mashindano hayo ambao sasa wanacheza Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Kuuza wachezaji ambao wamepatikana kupitia mashindano haya ni jambo la kujivunia kama timu, hivyo Kombe la Mapinduzi lina faida kubwa sana kwetu,” anasema.

MLAND 04

“Hatuwezi kununua wachezaji wa nje ya Zanzibar kwa ajili ya mashindano haya kwani wageni watapata uzoefu zaidi kuliko wazawa, hivyo tunawapa wazawa fursa hii waitumie kuongeza uzoefu.”

Anaeleza kuwa, Mlandege imeingia kwenye rekodi ya timu inayopendwa zaidi Zanzibar na nje kupitia mashindano hayo kutokana na kile inachokifanya ndani ya uwanja.

China anasema hii ni hatua nyingine inayotazamiwa na timu hiyo katika kufikia malengo na mipango yao kuwa katika mustakabali mzuri.

MASTAA WAO

Mlandege wakati inabeba ubingwa wa mwaka 2024 iliichapa Simba bao 1-0, mfungaji alikuwa Joseph Akandwanaho ambaye sasa yupo TRA United. Pia kulikuwa na mshambuliaji Abdallah Idd ‘Pina’ aliyetimkia Pamba Jiji.

Inaingia katika michuano hii ikiwa haina nyota wake hao, lakini bado ipo imara kutokana na wale walipo hivi sasa wakiendelea kufanya vizuri katika Ligi Kuu Zanzibar.

Licha ya kwamba Mlandege ipo nje ya nafasi tano bora katika msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar msimu huu ikiwa ndiyo bingwa mtetezi, lakini inalitolea macho Kombe la Mapinduzi ikiwa ni sehemu ya kurudisha morali ambayo ligi ikiendelea, ikiwashe zaidi.

Ndani ya Mlandege, kuna mastaa kama Mussa Hassan ‘Mbappe’, Yusuf Suleiman ‘Jussa’ na Aimar Hafidh ‘Haaland’ ambao ni miongoni mwa wale wanaofanya vizuri.

MLAND 05

Mastaa hao sambamba na wengine wanaounda kikosi cha timu hiyo, wamepania kufanya kweli na kuiheshimisha Zanzibar kwa kulibakisha tena taji ardhi ya nyumbani.

Kombe la Mapinduzi tangu mara ya mwisho kuvuka maji 2022 likibebwa na Simba ya Jijini Dar es Salaam, limeendelea kubaki Zanzibar kwa kubebwa na Mlandege mwaka 2023 na 2024, kisha 2025 ikawa zamu ya Zanzibar Heroes.

MASHABIKI MZUKA MWINGI

Katika ladha ya soka, mashabiki huwezi kuwaweka mbali kwani wao hutajwa kuwa ni mchezaji wa 12 kutokana na sapoti wanayotoa kwa wachezaji wao.

Mashabiki wa Mlandege wana mzuka pindi timu yao inapokuwa uwanjani ikisaka ushindi kiasi cha wao wenyewe kusema huwa wanaumia kuliko wachezaji.

Huo ni msemo maarufu unaotumiwa na mashabiki wa timu hiyo kwenye kuipa hamasa wachezaji kufanya vizuri wakiwa uwanjani.

Kawaida ya mashabiki hao kuitika na kutoa hamasa kwa wachezaji, ndiyo inawafanya mechi zao nyingi zinapochezwa hujaza watazamaji wengi zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *