Diwani wa Kata ya Chanika Wilaya ya Handeni Mjini, Mkoani Tanga, Dkt. Habibu Mbota, amepiga marufuku tabia ya kuweka viroba vya taka barabarani, akieleza kuwa kitendo hicho kinachafua mazingira na kuhatarisha afya za wananchi.

Hatua hiyo imetolewa wakati wa zoezi la usafi wa mazingira la Jumamosi ya mwisho wa mwezi, ambapo Diwani huyo alijumuika pamoja na vijana na wafanyabiashara wa kata hiyo kufanya usafi katika maeneo mbalimbali.

Katika zoezi hilo, baadhi ya kero zilizoibuliwa ni pamoja na ucheleweshaji wa magari ya taka pamoja na uwekaji wa viroba vya takataka katika barabara za kata hiyo, hali inayosababisha mlundikano wa taka na kuharibu mandhari ya mji.

Kutokana na hali hiyo, Mbota aliwaelekeza Maafisa Mazingira kuacha mara moja utaratibu wa kusafisha mitaro na kuweka viroba vya taka barabarani, badala yake watafute njia salama na rafiki kwa mazingira katika zoezi la usafi wa mji.

Aidha,amewahimiza wananchi kuendelea kulipia michango ya usafi katika maeneo yao ili kuwezesha huduma hiyo kufanyika kwa ufanisi, Vilevile, vilevile ameahidi kuishauri Halmashauri kuona umuhimu wa kununua gari la taka ili kupunguza ucheleweshaji wa ukusanyaji wa taka.

Diwani Mbota amesema hatua hiyo itasaidia kuepuka mlundikano wa taka, kulinda mazingira na kupunguza hatari ya mlipuko wa magonjwa katika kata ya Chanika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *