MSHAMBULIAJI wa Pamba Jiji, Abdallah Idd ‘Pina’ amekamilisha uhamisho wa kujiunga na Muembe Makumbi City ya Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), baada ya kushindwa kuwika Ligi Kuu Bara akiwa na kikosi hicho cha TP Lindanda.

Nyota huyo aliyejiunga na Pamba msimu huu akitokea Mlandege ya Zanzibar na kusaini mkataba wa miaka miwili, alitabiriwa kufanya mambo makubwa kutokana na alichofanya msimu wa 2024-2025, akiwa na kikosi hicho, ingawa mambo yamekuwa tofauti.

Msimu uliopita wa 2024-2025 katika ZPL, Pina aliibuka mfungaji bora baada ya kufunga mabao 21, kupitia mechi 22, alizozicheza, huku akiasisti mengine 12, japo akiwa na Pamba hajafunga bao lolote la Ligi Kuu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Pamba Jiji, Ezekiel Ntibikeha amesema baada ya mchezaji huyo kukosa muda mrefu wa kucheza wameona ni vyema wamtafutie timu itakayompa nafasi ya kuonekana zaidi.

“Moja ya kitu tulichofanikiwa kwa kiasi kikubwa ni kuboresha kikosi chetu katika kila eneo kwa kuleta wachezaji wazuri imekuwa ngumu kwake kuendana na kasi ya Ligi Kuu Bara, lakini bado tuna matumaini naye huko mbeleni,” amesema Ntibikeha.

Uwepo wa washambuliaji wengine wakiwemo, Mkenya Mathew Momanyi aliyefunga mabao saba ya Ligi Kuu Bara msimu uliopita na Abdoulaye Camara aliyekuwa na manne, umechangia pia kwa kiasi kikubwa nyota huyo kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara.

Ujio pia wa Mganda Peter Lwasa aliyejiunga na kikosi hicho cha Pamba akitokea Kagera Sugar, ambaye msimu huu tayari amefunga mabao matatu ya Ligi Kuu Bara huku akionyesha kiwango kizuri, kumechangia kwa nyota huyo kutolewa kwa mkopo.

Pina aliyeianza safari ya soka mwaka 2015 amewahi kuzichezea pia timu za Magomeni, Gulioni, Jang’ombe Boys, Polisi Tanzania, Kipanga, Kundemba, Mlandege na sasa Muembe Makumbi City, huku za nje ni za Alzakhir ya Dubai na Chaux Sport ya DR Congo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *