Unguja. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla ameiagiza Wizara ya Afya kuhakikisha wanatoa ajira kwa vijana wazawa wenye sifa za kutoa huduma za afya kisiwani hapa.

Hayo ameyasema leo Jumamosi Desemba 27, 2025 wakati wa uwekaji Jiwe la msingi la kituo cha Afya Tumbatu ikiwa ni shamrashamra za maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Hemed amesema uwepo wa wataalamu wazawa watafanikisha kutoa huduma kwa wagonjwa wakati wote ikiwemo huduma za dharura kwa mama wajawazito na wagonjwa wengine kuanzia ngazi ya jamii, vituo vya afya hadi hospitali kuu.

Pia, amesema kituo hicho kitakapokamilika kitaimarisha upatikanaji wa huduma za afya za msingi ikiwemo huduma za mama na mtoto, huduma za dharura, maabara pamoja na huduma za kinga na tiba.

“Naugiza uongozi wa wizara kuweka kipaumbele cha ajira kwa vijana wazawa wenye sifa za kuajirika na uwezo wa kutoa huduma za afya kwa wananchi wakati wote wanapohitajika,” amesema. 

Vilevile, Hemed amesema uamuzi wa kujengwa kituo hicho cha afya ni hatua muhimu ya Serikali ya kuimarisha miundombinu ya afya kwa lengo la wananchi wake kupata huduma kwa ukaribu katika mazingira bora yanayolingana viwango.

Hemed, amefahamisha kuwa Serikali inaendelea na shabaha yake ya kuweka mifumo imara katika Sekta ya afya ikiwema mfumo wa rufaa ambapo tayari imekamilisha ujenzi wa hospitali za Wilaya zinazoendelea kutoa huduma kwa wananchi katika Wilaya zote za Zanzibar.

Amesema, hatua nyengine ni ujenzi wa hospitali za Mikoa kati ya minne iliyobaki, ujenzi wa Hospitali kubwa na ya kisasa ya Binguni pamoja na kuifanyia matengenezo hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja huku hospitali ya Mkoa ya Lumumba ikiendelea kutoa huduma kwa wananchi wa Zanzibar.

Makamu huyo, amewataka wazanzibari kuendelea kuyalinda na kuyaenzi Mapinduzi  ya Zanzibar ya mwaka 1964, kudumisha amani na mshikamano ambao ndio nyenzo muhimu katika kuyafikia maendeleo wanayoyatarajia.

Akitoa taarifa ya kitaalamu, Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar,  Dk Mngereza Mzee Miraji amesema mradi wa kituo hicho unagharimu Sh6.4 billioni na unajengwa kwa fedha za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) chini ya mkandarasi Simba Developer Limited.

Pia, amesema Wizara hiyo imejikita kwenye utekelezaji wa vipaumbele vitano vya serikali katika kuimarisha huduma za afya ya msingi kwa jamii ambavyo ni kuwa na miundombinu rafiki ya utoaji huduma, kuwa na watumishi wenye sifa na uwezo wa kutoa huduma kwa wakati, upatikanaji wa dawa na vifaa tiba na utoaji wa huduma za Afya kwa kutumia mifumo ya tehama.

Amesema, ujenzi huo utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kuhudumia wakazi 18,366 wa kisiwa cha Tumbatu,  kitakuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa zaidi ya 30 kwa wakati mmoja na kutoa huduma kwa masaa 24 ya kazi.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Ungaja, Gallos Nyimbo ameiomba Serikali kujengwa kwa soko kubwa na la kisasa katika kisiwa ya Tumbatu ili kukifungua kibiashara na kukuza uchumi kwa wananchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *