Mbarali. Mbunge wa Mbarali mkoani Mbeya, Bahati Ndingo amesema wameweka mikakati ya kutatua migogoro ya ardhi baina ya wananchi na wawekezaji, hususan inayohusisha mipaka ya mashamba katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.

Ndingo amesema kwa sasa wanasubiri idhini ya Serikali ili kushirikisha wataalamu kwa ajili ya kuhakiki upya michoro ya ramani na mipaka katika maeneo yenye migogoro ya muda mrefu na ya muda mfupi, sambamba na kuwashirikisha wananchi husika.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumamosi, Desemba 27, 2025, Ndingo amesema migogoro ya ardhi eneo la Mbarali ni mingi na imekuwa chanzo cha malalamiko kwa wananchi.

“Mbarali migogoro ya ardhi ni mingi, lakini sasa tunasubiri kupata idhini kutoka mamlaka husika ili kuhakiki upya michoro ya ramani na mipaka na hatimaye kumaliza matatizo haya,” amesema mbunge huyo.

Amesema uwepo wa migogoro hiyo unasababisha baadhi ya wananchi kuichukia Serikali yao, hali inayomlazimu kiongozi kama mbunge kusaka suluhisho la kudumu.

“Kwa sasa siasa zimekwisha, tuko kwenye utekelezaji wa kuhakikisha migogoro isiyo na majibu inafikia mwisho, ikiwemo ile inayohitaji kushughulikiwa katika ngazi za kitaifa,” amesema.

Katika hatua nyingine, Ndingo amesema Wilaya ya Mbarali pia inakabiliwa na changamoto ya ubovu wa barabara, akieleza kuwa wameweka mikakati ya kuhakikisha bajeti inapotengwa, barabara zinajengwa kwa viwango stahiki badala ya kuboreshwa kwa muda mfupi.

Amesema makandarasi watakaopata zabuni watalazimika kujipanga na kufanya kazi kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa, huku akibainisha kuwa takribani asilimia 90 ya barabara za vijijini bado haziridhishi.

“Tunahitaji kuona barabara za Mbarali zinakuwa na ubora unaotakiwa, ikiwemo barabara ya Lujewa–Madibira ambayo ni mbovu na imekuwa kilio kikubwa cha wananchi,” amesema.

Ameongeza kuwa kuelekea kipindi cha bajeti, fedha kwa upande wa wilaya hiyo zimeongezeka kwa kiasi kikubwa kwa kuzingatia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi, huku kipaumbele kikitolewa katika ujenzi wa barabara za mitaa na zile zinazosimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads).

Wakati huohuo, Ndingo amesema ataifuatilia kwa karibu miradi yote inayotekelezwa na Serikali wilayani humo ili kudhibiti utekelezaji wa miradi isiyojengwa kwa ubora unaokidhi viwango.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Raymond Mweli amesema katika kuhakikisha migogoro ya ardhi inamalizika, halmashauri imeanza mkakati wa kuwasajili wananchi na kuwapatia hati miliki.

“Aidha, nimeagiza wataalamu kwenda kwa wananchi kusikiliza na kutatua kero zao, jambo ambalo nimelisisitiza tangu nilipoingia katika nafasi hii,” amesema Mweli.

Ameongeza kuwa halmashauri imetenga Sh1 bilioni kwa ajili ya kununua mtambo wa kuchonga barabara za pembezoni, hatua inayolenga kuongeza kasi ya matengenezo ya barabara na makusanyo ya ndani yatakayochangia miradi ya maendeleo.

“Hadi sasa tumepeleka Sh1.4 bilioni kutekeleza miradi ya maendeleo, ikiwa ni sehemu ya asilimia 60 ya fedha zilizokusudiwa, lengo ni kutekeleza maagizo ya Serikali,” amesema.

Kauli za wananchi

Mkazi wa eneo hilo na dereva wa bajaji, Daniel Joel amesema uchakavu wa barabara ya Lujewa–Ubaruku imekuwa kero kubwa kwa watumiaji wa vyombo vya moto huku akiiomba Serikali kufanya maboresho ili kupunguza gharama na hasara za mara kwa mara.

“Kimsingi barabara hii ni mbovu sana. Hatua ya halmashauri kununua mtambo wa kuchonga barabara itasaidia kupunguza umbali na muda wa safari, hususan katika maeneo ya pembezoni,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *