Unguja. Ujenzi wa nyumba 3,000 za makazi bora unatajwa kuleta mabadiliko kwa wananchi wa Zanzibar, ikiwa ni hatua ya kuendeleza makazi bora.

Jiwe la msingi la nyumba hizo zinazojengwa Chumbuni, Mkoa wa Mjini Magharibi, limewekwa leo Desemba 27, 2025 katika shamrashara za Mapinduzi ya Zanzibar.

Nyumba hizo zinajengwa kwa awamu, ya kwanza ikihusisha ujenzi wa 1,095 kazi inayotekelezwa na kampuni kutoka China kwa gharama ya Sh145.9 bilioni.

Akizungumza wakati wa uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa nyumba hizo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar mstaafu, Balozi Seif Ali Idd, amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa dhamira na ndoto za Rais wa kwanza wa Zanzibar, hayati Abeid Amani Karume.

Balozi Seif, aliwakilishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ, Idrissa Kitwana Mustapha.

“Mzee Karume alipenda kuona wananchi wakiishi katika makazi bora na ndiyo maana baada ya mapinduzi alijenga nyumba za Michenzani, Kilimani na kwingineko akawagawia bure waishi kwa amani,” amesema.

Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha kila mwananchi anaishi kwenye makazi bora na ya kisasa, hivyo itaendelea kujenga nyumba kusaidia upatikanaji wa makazi safi, salama na yenye hadhi.

Ujenzi wa nyumba 300 za makazi ukiendelea eneo la Chumbuni Mkoa wa Mjini wa Magharibi, Zanzibar. Picha na Jesse Mikofu

Amesema asilimia 40 ya nyumba hizo zinazojengwa ni kwa ajili ya wananchi wa hali ya chini.

Balozi Seif, amesema miongoni mwa vitu vinavyompa thamani binadamu ni kuwa na makazi bora, kwani yanaleta utulivu na uimara kimwili na kiakili.

Amewataka wananchi kuendelea kuwa na umoja na mshikamano ili kudumisha amani iliyopo kama ambavyo malengo ya mapinduzi yalikuwa.

Bila ya kuwa na amani na utulivu, ameeleza hata miradi ya maendeleo haitakuwa na maana kwa sababu hakutakuwa na nafasi ya kuitekeleza.

“Pasipo amani na utulivu hakuna maendeleo tutakayopata, kwa hiyo niwaombe wananchi wenzangu tuendelee kuitunza amani tuliyonayo ili kurithisha vizazi hadi vizazi,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Zanzibar, Sultan Suleiman, amesema huo ni miongoni mwa miradi ya kimkakati kuhakikisha kuna nyumba nyingi za makazi bora Zanzibar.

Amesema mradi wa nyumba 3,000, asilimia 40 zitakuwa kwa ajili ya wananchi wa kipato cha chini.

Amesema nyumba hizo hazitakuwa na gharama za kodi kwa kuwa Serikali imeziondoa ili kuweka wepesi katika upangishaji na umiliki.

“Huu ni mradi wa kimkakati, nyumba hizi zitaleta chachu ya makazi bora, zitaleta haiba nzuri ya miji kwa kuanzisha miji ndani ya miji,” amesema.

Sultani amesema mradi huo utakuwa chachu ya maendeleo kijamii na kiuchumi kwa manufaa ya wananchi na Serikali kwa ujumla.

Hata hivyo, amesema katika utekelezaji wa mradi huo wamekutana na changamoto kadhaa, ikiwemo ya vifaa kuchelewa bandarini na malipo ya fidia kwa wananchi waliotakiwa kupisha eneo kwa ajili ya mradi huo.

Mwenyekiti wa kampuni inayotekeleza mradi huo inayojulikana kama Zanzibar and Weihai Huatan Ltd, Dk Lisa Wang, amesema wanafarijika kuwa sehemu ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ya Serikali.

Amesema ahadi yao ni kutekeleza mradi huo kwa kiwango kinachotakiwa ili kufikia matakwa ya Serikali.

Amesema ikiwa kampuni yenye uzoefu katika miradi ya namna hiyo, watahakikisha unakamilika kwa viwango vinavyotakiwa.

Naibu Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Salha Mohamed Mwinjuma, amesema mradi huo ni wa kimkakati na unapojengwa, utabadilisha madhari ya eneo hilo ambalo lilikuwa likionekana kama shamba na kuwa mji wa kisasa.

Kwa mujibu wa Salha, katika eneo hilo kutakuwa na huduma zote zikiwamo shule, hospitali na nyingine kama hizo.

“Hapa utakuwa mji wa kisasa, huduma zote zitapatikana hapa zikiwamo shule na hospitali. Hakuna mtu kwenda nje kufuata huduma hizo,” amesema.

Amesema ukubwa wa mradi huo unazidi nyumba zote zinazomilikiwa na wizara hiyo kwa sasa zikichanganywa kwa pamoja.

Kwa sasa inazinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi miradi zaidi ya 170 Unguja na Pemba, kabla ya kuhitimishwa katika sherehe za Mapinduzi zitakazofanyika Januari 12, 2026, siku yalitokea Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *