Liverpool, England. Watoto wa staa wa zamani wa Liverpool Diago Jota leo wamerejea kwenye Uwanja wa Anfield kama mascots wa mchezo wa Ligi Kuu England kati ya Liverpool na Wolves zikiwa ni timu mbili za England ambazo alizichezea baba yao kabla hajafariki.

Dinis na Duarte, wawili kati ya watoto watatu wa Jota na Rute Cardoso, wameingia katika Uwanja wa Anfield kabla ya mechi kuanza, katika tukio ambalo limekuwa la kihistoria.

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa timu hizo mbili kukutana tangu mchezaji huyo wa kimataifa wa Ureno mwenye umri wa miaka 28 alipofariki dunia katika ajali ya gari Kaskazini-Magharibi mwa Hispania mwezi Julai, pamoja na ndugu yake André Silva, mwenye umri wa miaka 25.

Jota alikuwa akisafiri kurejea Liverpool kwa ajili ya kuanza mazoezi ya maandalizi ya msimu mpya na msiba huo ulisababisha wimbi kubwa la majonzi kutoka kwa jumuiya ya soka duniani kote.

Katika maelezo yake ya programu ya kabla ya mechi kuelekea mchezo wa mwisho wa nyumbani wa mabingwa msimu huu, kocha Arne Slot alisema anatumaini mapenzi yaliyoonyeshwa kwa Diogo Jota yataweza kuleta faraja kwa familia yake.

“Kutafakari yote yaliyotokea katika miezi 12 iliyopita kunazua hisia nyingi tofauti, lakini ni kawaida wakati huu wa mwaka kuangalia yaliyojiri,” alisema kocha wa Liverpool.

“Kufanya hivyo kunanifanya niwaze zaidi familia ya Diogo Jota, hasa kwa kuwa hii itakuwa Krismasi yao ya kwanza bila yeye.

“Sio nafasi yangu kuwaambia wanapaswa kutafuta wapi faraja kama hilo linawezekana lakini ninaweza tu kutumaini kuwa hisia za upendo na mapenzi ambazo Diogo bado anazalisha zitawapa faraja fulani.”

Rob Edwards na wachezaji wa Wolves walitembelea mchoro (mural) wa aliyekuwa mshambuliaji wa Liverpool nje ya Anfield siku ya Boxing Day ili kutoa heshima zao.

Jota alijiunga na Wolves kwa mkopo kutoka Atletico Madrid mwaka 2017 kabla ya kujiunga nao moja kwa moja mwaka uliofuata baada ya kusaidia timu hiyo kupanda daraja.

Baada ya kung’ara kwa misimu miwili zaidi katika eneo la West Midlands, ambapo alifunga mabao 44 katika mechi 131, Jurgen Klopp alimchukua Jota mwaka 2020. Aliendelea kushinda taji lake la kwanza la Ligi Kuu ya England akiwa Liverpool katika msimu wa kwanza wa Slot mapema mwaka huu. Pia alishinda Kombe la FA na Kombe la Ligi mwaka 2022.

Ilifichuliwa mapema msimu huu kuwa wamiliki wa Liverpool, FSG, wamejitolea kuendelea kumtunza Rute Cardoso, mjane wa Jota, pamoja na watoto wao watatu, na wataheshimu mkataba wake wote uliobaki, unaoripotiwa kuwa na thamani ya takribani pauni 140,000 kwa wiki. Jota alikuwa na miaka miwili iliyosalia kwenye mkataba wake.

Liverpool pia ilistaafisha jezi namba 20 ya Jota katika timu zote msimu wa kiangazi, huku mashabiki wakiendelea kumuenzi kwa kuimba wimbo wake katika dakika ya 20 ya kila mechi ya nyumbani msimu huu.

Wolves watakuwa wenyeji wa mchezo wa marudiano tarehe 4 Machi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *