
MSHAMBULIAJI wa zamani wa Dodoma Jiji, Waziri Junior anatarajiwa kuanza kuitumikia timu hiyo kupitia dirisha dogo la usajili litakapofunguliwa Januari Mosi, 2026 baada ya awali nyota huyo kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi mwishoni mwa msimu uliopita.
Nyota huyo amerejea tena Dodoma Jiji baada ya kuondoka Februari 7 mwaka huu kwenda kujiunga na Al-Minaa ya Ligi Kuu ya Iraq kwa mkopo wa miezi sita, ingawa hakuitumikia timu hiyo baada ya Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kuchelewa kutoka.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari wa Dodoma Jiji, Moses Mpunga amesema uongozi wa timu hiyo unaendelea kufuatilia kwa ukaribu ITC ya nyota huyo ili aweze kukitumikia kikosi hicho, baada ya kukaa nje kwa muda mrefu tangu aliporejea.
“Wapo wachezaji wengine tuliowasajili dirisha kubwa lililopita ila hadi sasa hawajacheza kwa sababu ITC zao zilichelewa, naamini muda sio mrefu kila kitu kitakamilika na wataanza kuonekana Ligi Kuu Bara itakaporejea tena,” amesema Mpunga.
Nyota huyo alijiunga na Dodoma Jiji kwa mkataba wa miaka miwili, akitokea KMC, ingawa aliitumikia kwa miezi sita baada ya kupata dili la kwenda kucheza Iraq, ambayo ingemsajili moja kwa moja ikiwa ingevutiwa na uwezo wake.
Waziri hadi anaondoka Dodoma Jiji, alikuwa amefunga bao moja tu la Ligi Kuu Bara katika ushindi wa kikosi hicho wa 2-0, dhidi ya TRA United zamani Tabora United, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Oktoba 2, 2024.
Msimu wa 2024-2025, haukuwa mzuri zaidi kwa nyota huyo kutokana na kuandamwa na majeraha ya mara kwa mara, ingawa msimu bora kwake ni wa 2023-2024, alipokuwa KMC ambapo alishika nafasi ya tatu ya wafungaji bora, baada ya kufunga mabao 12.
Katika msimu huo, Waziri alizidiwa na kiungo mshambuliaji nyota wa Azam, Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyefunga mabao 19 na kinara nyota, Stephane Aziz KI aliyekuwa Yanga aliyefunga 21, ingawa kwa sasa anaichezea Wydad Casablanca ya Morocco.
Baada ya kuichezea Al-Minaa, mshambuliaji huyo amekuwa ni Mtanzania wa pili kucheza soka la kulipwa katika Ligi Kuu ya Iraq, akifuata nyayo za nyota wa zamani wa kikosi cha Yanga, Saimon Msuva ambaye kwa sasa anaichezea Al-Talaba.