WAKATI dirisha dogo la usajili likitarajiwa kufunguliwa Alhamisi mabosi wa Fountain Gate wameanza mazungumzo ya kupata saini ya mshambuliaji nyota wa kikosi cha Mbeya Kwanza inayoshiriki Ligi ya Championship, Boniface Mwanjonde.

Mwanaspoti linatambua, jana Jumamosi mabosi wa Fountain Gate walikuwa wanamfuatilia kwa ukaribu akiwa na Mbeya Kwanza, iliyokuwa inacheza na Gunners, katika mechi ya Championship iliyokuwa inachezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

Chanzo kutoka ndani ya timu hiyo, kimeliambia Mwanaspoti, mshambuliaji huyo ambaye kwa sasa amekuwa na kiwango kizuri na Mbeya Kwanza, ni miongoni pia mwa nyota wanaosakwa dirisha hili la Januari, ili kwenda kukiongezea nguvu kikosi hicho.

“Kocha wetu, Mohamed Ismail ‘Laizer’, amempendekeza asajiliwe na sisi hatuna tatizo juu ya mapendekezo yake ndio maana tumeanza kumfuatilia kwa ukaribu kumuangalia na kufanya mazungumzo rasmi na klabu inayommiliki,” kilisema chanzo hicho.

Nyota huyo hadi sasa ameonyesha kiwango bora akiwa na Mbeya Kwanza aliyoifungia mabao manane, huku akiwa ni miongoni mwa wachezaji wawili waliofunga (hat-trick) msimu huu katika Ligi ya Championship, sambamba na Obrey Chirwa wa Kagera Sugar.

Fountain Gate inasaka mshambuliaji wa kuongeza nguvu katika timu hiyo, baada ya kucheza mechi 10 za Ligi Kuu Bara msimu huu, huku safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho ikiwa imefunga mabao manne tu na kuruhusu mabao 12.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *