
Doumbouya ni kamanda wa zamani wa vikosi maalum. Alikamata madaraka katika mapinduzi ya kijeshi ya 2021 na anagombea kiti cha urais pamoja na wagombea tisa ambao hawana ushawishi. Umoja wa Mataifa unasema kipindi cha kuelekea uchaguzikilikumbwa na matukio ya vitisho na vikwazo dhidi ya uhuru wa raia. Kiasi ya watu milioni saba wamesajiliwa kupiga kura nchini humo. Matokeo ya awali yanatarajiwa kuanza kutolewa saa 72 baada ya vituo vya kupigia kura kufungwa. Doumbouya alimuondoa madarakani Rais Alpha Conde miaka minne iliyopita.
Awali, alikuwa amefuta uwezekano wa kugombea kwenye uchaguzi huo. Hata hivyo, katiba mpya iliyopitishwa mwezi Septemba iliondoa marufuku kwa viongozi wa kijeshi kugombea nyadhifa za umma. Pia iliongeza muhula wa urais hadi miaka saba. Licha ya rasilimali nyingi za madini za Guinea — ikiwa ni pamoja na kuwa muuzaji mkubwa zaidi wa bauxite duniani, inayotumika kutengeneza alumini — zaidi ya nusu ya jumla ya watu milioni 15 wanakabiliwa na viwango vya umaskini na ukosefu wa uhakika wa chakula, kulingana na Mpango wa Chakula Duniani.