MAKUNDI ya watalii kutoka barani Ulaya na Asia yakitumia ndege binafsi yameendelea kumiminika katika msimu huu wa chini wa utalii kwenda kuangalia vivutio vya utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.
Hali hiyo ni tofauti na miaka kadhaa ya nyuma katika kipindi cha miezi mitatu ya mwisho wa mwaka ambacho huitwa kipindi cha chini cha utalii kwenda kutalii katika hifadhi hizo kwani watalii wanakuwa wachache kutokana na baadhi yao kuamua kukaa nchini kwao kusherehekea sikukuu hizo za mwisho wa mwaka.
Mmoja wa wakuu wa waongoza watalii wa Kampuni ya Utalii ya Cosheni Safari, Bariki Mseli amesema Desemba 23, mwaka huu saa 11.05 jioni kampuni yake imepokea watalii 106 kutoka Israel waliokwenda kutua moja kwa moja katika Kiwanja kidogo cha Ndege cha Seronera kilichopo ndani ya Hifadhi kubwa na yenye sifa lukuki duniani ya Serengeti.

Mseli amesema kundi hilo la watalii kutoka nchini Israel mbali ya kutalii na kuangalia vivutio pia katika ujio wao wameamua kutumia kipindi hiki kusherehekea sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya. SOMA: Mambo yanayoipa Hifadhi ya Ngorongoro upekee duniani
Amesema mbali ya hilo pia alipokea watalii wa makundi tofauti mawili ya watu 86 kutoka Japan na Hispania wakiwa katika ndege binafsi za kukodi nao waliamua kwenda katika Hifadhi ya Serengeti kutalii na kusherehekea sikukuu ya krismasi kabla ya kwenda Zanzibar kutalii katika fukwe za Bahari ya Hindi.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Utalii ya Tanzania Specialist, Agael Mollel amesema kampuni yake katika msimu huu wa utalii wa chini imefanya kazi nyingi na kupokea makundi ya watalii kutoka nchini Uingereza, Ufaransa na Hispania. Amesema msimu huo umechanganya tofauti na miaka ya nyuma na kuona kama ni msimu wa juu wa utalii kwa kipindi cha miezi mitatu ya mwisho wa mwaka.
Mollel amesema watalii wanamiminika nchini hususani Kiwanja kidogo cha Ndege cha Seronera kilichopo ndani ya Hifadhi ya Serengeti na kuwataka wale wenye kudhani hali siyo shwari nchini waondokane na mawazo hayo potofu kwani kazi inafanyika usiku na mchana.

Muongoza watalii wa Kampuni ya utalii ya Kilimanjaro Travel, Andew Mushi amesema wao hawajui kama huu ni msimu wa chini wa utalii bali wanaona kama kawaida kwani wamekuwa wakipokea wageni wengi kwa nyakati tofauti na kuwapeleka Serengeti, Ngorongoro na Zanzibar kutalii.
Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Serengeti, Choya Choya alisema pamoja na kupokea watalii wengi katika hifadhi hiyo pia wamejipanga kikamilifu kulinda usalama wa watalii wa nje na ndani wanaomiminika katika hifadhi hiyo ili waweze kutalii na kusherehekea vyema sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya kwa usalama na amani.
Kwa upande wake Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Walter Mairo amesema makundi ya watalii yamekuwa yakimiminika katika hifadhi hiyo na wengine kuamua kutumia nafasi hiyo kusherehekea sikukuu msimu wa sikukuu ndani ya hifadhi hiyo.