MWEKEZAJI maarufu wa Marekani, Robert Kiyosaki, amesisitiza wito wake wa kuwekeza katika madini ya thamani na fedha za kidijitali akidai kuwa dola ya Marekani ipo hatarini kupoteza nguvu. Kiyosaki amesema kundi la BRICS limetangaza sarafu yake mpya yenye mgongo wa dhahabu, na kuwaonya wahifadhi wa dola ya Marekani kuhusu hatari ya mfumuko mkubwa wa bei.
Amesema: “Kwaheri dola ya Marekani! Milikini dhahabu, fedha, Bitcoin na Ether. Kaeni macho, endeleeni kufuatilia. Wanaohifadhi dola watakuwa wahanga wakubwa.” Madai haya yameibua mjadala kuhusu uwezekano wa kuanzishwa mbadala wa dola ya Marekani, licha ya kuwa hakuna tangazo rasmi limefanywa na nchi wanachama wa BRICS.
Tetesi ziliongezeka baada ya Vladimir Putin kuonekana akishika mfano wa “noti ya BRICS” katika Mkutano wa Kazan Oktoba 2024, ingawa maafisa wa ngazi za juu wamesema kuwa hakuna mpango wa haraka wa kuzindua sarafu hiyo. SOMA: Indonesia yachangia Dola Bilioni 1 Benki ya Maendeleo BRICS
Viongozi wa BRICS akiwemo Putin, wamesema kuwa lengo si kuachana kabisa na dola ya Marekani au mfumo wa SWIFT, bali kuunda njia mbadala zitakazowezesha kutumia sarafu za ndani katika miamala ya kimataifa. Putin ameongeza kuwa hatua hiyo itafanywa kwa umakini na tahadhari, huku nchi wanachama zikitegemea uwezo wa Benki ya Maendeleo ya BRICS kutekeleza mpango huo.
