
Jeshi la Iran limeonya kwamba, hatua yoyote ya uadui kutoka kwa maadui itakabiliwa na jibu kali, huku likisisitiza juu ya utayarifu wake wa kulilinda na kulihami taifa.
Jeshi la Iran limetoa taarifa hiyo kwa mnasaba wa kumbukumbu ya hamasa ya tarehe 9 Dey mwaka 1388 Hijria Shamsia sawa na Disemba 30 mwaka 2009. Wananchi wanamapinduzi walijitokeza kushiriki maandamano ya kutetea thamani za Kiislamu na Mapinduzi.
Katika taarifa hiyo, Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limesisitiza tena kujitolea kwake kulilinda taifa la Iran na kukabiliana na hatua yoyote ghalati ya maadui.
Taarifa hiyo imeeleza kwamba, Jeshi la Iran, pamoja na matawi mengine ya Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu, linaendelea kufungamana na “umoja mtakatifu” wa watu wa Iran na hamasa kuu ya Dey 9.
Likirejelea hali ya sasa na matukio ya hivi karibuni katika eneo, Jeshi la Iran limesema limejiandaa kamilifu kutetea taifa jasiri la Iran na kulinda uhuru na mamlaka ya kujitawala Iran, na Mfumo wa Kiislamu unaotawala hapa nchini.
Taarifa hiyo imesisitiza kwamba, Jeshi la Iran linafanya kazi chini ya uongozi wa busara wa Amiri Jeshi Mkuu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, na kutangaza kwamba linasimama imara na thabiti kama mlima dhidi ya maadui.
Katika maandamano ya mamilioni ya watu mnamo tarehe 9 Dei mwaka wa Kiirani 1388 sambamba na 30 Desemba 2009, wananchi wa Iran walitangaza bayana kujibari na wavunja sheria katika jamii.