Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amemsifu shahidi na kamanda wa vita dhidi ya ugaidi, Luteni Jenerali Qassim Soleimani na kumtaja kuwa “mbunifu wa Mhimili wa Muqawama” katika eneo Magharibi mwa Asia.
Sayyid Abbas Araqchi amesema haya alipohutubia mkutano wa kimataifa wa kuenzi urithi na yaliyofanywa na Luteni Jenerali Qassim ambaye aliuliwa shahidi na Marekani Januari 2020 akiwa safarini nchini Iraq.
“Haji Qassim alikuwa mbunifu wa Mhimili wa Muqawama katika eneo la Magharibi mwa Asia,” amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran.
Ameongeza kuwa: Katika kipindi nyeti cha sasa katika historia ya dunia, ambapo mfumo wa kimataifa umeporomoka na kuwa utaratibu unaotegemea mabavu, sera ya Iran ya kupigania haki ingali inapambana na ukandamizaji na dhulma ya madola ya kibeberu.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amesema: Wengi wanahisi mustakabali wa eneo hili kuwa chini ya “udhibiti wa Israel” lakini ukweli wa mambo katika eneo hili na ulimwenguni kwa ujumla unaonyesha kuwa Muqawama umekuwa hakika isiyopingika ya kijiografia na kisiasa, na moja ya pande kuu zenye ushawishi mkubwa katika kuunda mfumo wa siku zijazo wa eneo la Asia Magharibi.

Luteni Jenerali Qassim Soleimani aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu Mkuu wa Kikosi cha al Hashdu Shaabi cha Iraq na wanajihadi wenzao 8, waliuawa shahidi Januari 3 mwaka 2020 katika shambulizi la anga lililofanywa na jeshi vamizi na la kigaidi la Marekani katika uwanja wa ndege wa Baghdad nchini Iraq.
Binti wa Kamanda Soleimani, Zainab pia amehutubia mkutano huo wa kuenzi urithi wa kiongozi huyo wa Kambi ya Muqawama.