Katibu Mkuu wa shirika la kijeshi la NATO, Mark Rutte ameshikilia msimamo wa kutaka nchi za Ulaya ziendelee kuwa tegemezi kiulinzi kwa Marekani.

Rutte amesisitiza kuwa, nchi wanachama wa NATO zingali zinaweza kuitumainia Marekani, na kwamba mfumo wa ulinzi wa Ulaya haupasi kuwa wa kujitegemea na kujitenga na Marekani. Akizungumza katika mahojiano na shirika la habari la Ujerumani (DPA), Katibu Mkuu wa NATO ameeleza kwamba, Ulaya inapaswa ijigharimie zaidi kwa ajili ya usalama wake, lakini huku ikiendelea kuwa pamoja na Marekani. Rutte ameendelea kueleza: “nina uhakika kwamba Marekani inaiunga mkono NATO kikamilifu. Hakuna shaka yoyote kuhusu hilo”.

Katibu mkuu wa NATO ameeleza pia kuwa, hakubaliani na rai ya Trump kwamba Ulaya inapaswa ilibebe yenyewe jukumu la kujilinda kijeshi. Mark Rutte amedai kuwa, Washington itaendelea kujitolea kwa ajili ya bara hilo licha ya kukirejesha Marekani mnamo Oktoba mwaka huu kikosi chake cha kivita kutoka Romania pasi na kutuma kikosi mbadala. Hata hivyo, uamuzi huo unaonekana kama hatua ya kwanza na ya wazi kabisa ya kupunguza uwepo wa kijeshi wa Marekani barani Ulaya.

Mark Rutte

Rutte ametangaza msimamo wake huo wakati washirika wa Ulaya wanasubiri maamuzi ya Marekani, ambayo inatarajiwa kuondoa vyanzo vyake vya kijeshi kutoka Ulaya na kuvihamishia kwenye eneo la Indo-Pacific. Mnamo mwezi Machi 2025 pia, Marekani ilisimamisha usaidizi wake wa kijeshi kwa Ukraine na kuzilazimisha nchi za Ulaya kujaza pengo hilo.

Hii ni katika hali ambayo, hati ya mkakati wa usalama wa taifa ya Marekani iliyotolewa mwezi huu wa Desemba imezitaka waziwazi nchi za Ulaya zijilipie zenyewe gharama za ulinzi. Jambo hilo, pamoja na kuwepo tetesi za kupunguzwa ahadi ilizojifunga Marekani kutekeleza kwa ajili ya NATO, vimeufanya kuwa suala la dharura uharakishaji wa kuunda mfumo huru wa ulinzi wa Ulaya kwa ajili ya bara hilo.

Mara kadhaa, Rais Donald Trump wa Marekani amewataka washirika wa Washington wa Ulaya “wagawane mzigo wa ulinzi” na kubeba “jukumu kuu” la kulinda usalama wa bara hilo. Katika mkutano wa viongozi wa NATO uliofanyika The Hague Juni 2025, nchi za Ulaya ziliahidi kuongeza matumizi yao ya kijeshi hadi 3.5% ya Pato la Taifa na matumizi mengine yanayohusiana na ulinzi hadi 1.5%. Hadi sasa, ni Poland na Lithuania pekee ndizo zilizofikia kiwango cha 4%. Kulingana na makadirio ya NATO, zaidi ya nusu ya nchi wanachama zimebaki kwenye mpaka wa kiwango cha 2%.

NATO iliundwa kwa msingi wa kuwepo ushirikiano kati ya Marekani na nchi za Ulaya tangu kuasisiwa kwake mwaka 1949. Kutokana na nguvu zake za kijeshi, teknolojia ya hali ya juu, na bajeti kubwa ya kijeshi inayotumia, Marekani imekuwa mithili ya uti wa mgongo katika kubeba jukumu la uendeshaji wa muungano huo wa kijeshi wa Magharibi.

Trump

Inavyoonekana, msimamo uliotangazwa hivi karibuni na Katibu Mkuu wa NATO, Mark Rutte, kwamba Ulaya haipasi kujitegemea kikamilifu na kujitenga na Marekani katika uga wa ulinzi umetokana na sababu kadhaa:

Ya kwanza ni kwamba, uwezo wa kijeshi wa Marekani ni mkubwa mno kulinganisha na wa nchi za Ulaya kwa pamoja. Karibu 75% ya kiwango cha Pato la Taifa la nchi wanachama wa NATO kiko nje ya Umoja wa Ulaya, na sehemu yake kubwa ni ya pato la Marekani. Uwezo huo wa juu wa kiuchumi na kijeshi wa Washington unaifanya Ulaya iwe mhitaji wa ulinzi na usaidizi wa Marekani kwa ajili ya kukabiliana na vitisho kadhaa kikiwemo cha Russia na ugaidi wa kimataifa.

Lakini sababu ya pili ni kuwa, muundo wa kimkakati wa NATO umejengwa kwa msingi wa kutegemea uwepo wa Marekani. Washington sio tu ni mdhamini mkuu wa zana na teknolojia ya kijeshi, lakini pia ina mitandao mingi ya intelijensia na ya kilojistiki ambayo Ulaya peke yake haina uwezo wa kuipatia mbadala.

Kwa sababu hizo, Katibu Mkuu wa NATO anaamini kuwa, usalama wa Ulaya inapasa udhaminiwe kwa bara hilo kuwa bega kwa bega na Marekani, na si kwa kujitenga nayo.

Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa, ung’ang’anizi wa Katibu Mkuu wa NATO wa kutaka Ulaya iendelee kuwa tegemezi kiulinzi kwa Marekani unatokana na hali halisi ya nguvu za kijeshi na kiuchumi. Kwa mtazamo wake, Ulaya haiwezi kuhimili kikamilifu vitisho vya kimataifa bila ya Washington. Hata hivyo, utegemezi huo una matokeo hasi ambayo yanaweza kuubana uhuru wa kimkakati wa Ulaya na kuifanya idhurike pale yanapotokea mabadiliko katika sera za nje za Marekani. Na ndiyo kusema kwamba, mustakabali wa usalama wa Ulaya utaendelea kutegemea kiwango cha kujitolea Marekani kwa NATO na uwezo wa Ulaya yenyewe wa kuongeza mchango wake katika ulinzi wa pamoja…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *