
Begum Khaleda Zia, aliyekuwa waziri mkuu wa kwanza mwanamke wa Bangladesh na kiongozi mashuhuri katika siasa za taifa hilo, ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 80.
Chama cha Bangladesh Nationalist Party (BNP) kilitoa taarifa Jumanne kikisema: “Mwenyekiti wa BNP na waziri mkuu wa zamani, kiongozi wa taifa Begum Khaleda Zia, amefariki leo saa 12 alfajiri, mara tu baada ya sala ya Fajr.” Taarifa hiyo iliongeza: “Tunamuombea msamaha kwa Mola na tunawaomba wote kumkumbuka katika dua.”
Kifo chake kinahitimisha enzi iliyotawaliwa na ushindani mkali dhidi ya Sheikh Hasina, na nafasi yake ya kudumu kama alama ya upinzani na ustahimilivu.
Khaleda Zia alizaliwa Agosti 15, 1945 huko Jalpaiguri- wakati huo India ya Kikoloni, sasa Bengal Magharibi. Alikulia katika familia ya tabaka la kati. Mnamo 1960 aliolewa na Ziaur Rahman, afisa wa jeshi aliyepambwa kwa heshima na shujaa wa Vita ya Ukombozi ya Bangladesh ya 1971. Baada ya mumewe kutangaza uhuru wa Bangladesh na kisha kuwa rais mwaka 1977, akianzisha BNP, Khaleda Zia aliingia katika ulingo wa kisiasa.
Mwaka 1981, Rais Ziaur Rahman aliuawa katika jaribio la mapinduzi ya kijeshi. Tukio hilo lilimsukuma Khaleda Zia kuchukua uongozi wa BNP mnamo 1984.
Mnamo 1991, aliongoza chama chake kushinda uchaguzi na kuwa waziri mkuu wa kwanza mwanamke wa Bangladesh — na wa pili katika ulimwengu wa Kiislamu baada ya Benazir Bhutto wa Pakistan. Serikali yake ilijikita katika mageuzi ya kiuchumi, maendeleo ya miundombinu na kuimarisha uhusiano wa kimataifa. Alitumikia hadi 1996, wakati chama chake kiliposhindwa na Awami League ya Sheikh Hasina.
Khaleda Zia amefariki dunia alfajiri ya leo Desemba 30, akiwa amezungukwa na familia yake akiwemo mwanawe Tarique Rahman.
Anakumbukwa kama kinara aliyefungua njia kwa wanawake katika siasa na mtetezi wa demokrasia, ingawa alikosolewa kwa changamoto za utawala wake. Maisha yake yalikuwa kioo cha safari yenye misukosuko ya Bangladesh, kutoka mapambano ya uhuru hadi ndoto za demokrasia. Kifo chake kinahitimisha sura muhimu katika simulizi ndefu za kisiasa za taifa hilo.