London, England. Arsenal imeendelea kuonyesha dhamira ya kushindania taji la Ligi Kuu Englanda msimu huu baada ya kuichapa Aston Villa kwa mabao 4-1 kwenye Uwanja wa Emirates.

Ushindi huo uliifanya timu hiyo kuendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya pointi tano dhidi ya Aston Villa ambao walianza kulinganishwa na miujiza ya Leicester City ya mwaka 2016 lakini ndoto hizo zikivunjika ghafla baada ya rekodi yao ya ushindi wa mechi 11 mfululizo kukoma.

Licha ya kuanza kwa presha kubwa kutoka kwa Villa kipindi cha kwanza, Arsenal walionyesha ukomavu na uimara uliowafanya waonekane kama timu iliyokomaa kwa mbio za ubingwa. Hata kukosekana kwa kiungo wao tegemeo Declan Rice, bado vijana wa kocha Mikel Arteta walionyesha kiwango bora.

Mchezo huo ulishuhudiwa na nyota wa zamani wa Arsenal, Patrick Vieira na Martin Keown, waliokuwa sehemu ya kikosi kilichotwaa Ubingwa msimu wa 2003/04 bila kupoteza mchezo hata mmoja.

Villa walikuwa na nafasi ya kuongoza mapema baada ya Ollie Watkins kupoteza nafasi ya wazi kipindi cha kwanza. Baada ya mapumziko, kipa Emiliano Martinez alifanya kosa kubwa aliposhindwa kuokoa kona, hali iliyompa Gabriel bao la kwanza dakika chache baada ya kipindi cha pili kuanza.

Dakika nne baadaye, Martin Zubimendi aliifungia Arsenal bao la pili baada ya pasi maridadi ya nahodha Martin Odegaard, na hapo mchezo ulianza kuelemea upande mmoja. Leandro Trossard aliongeza bao la tatu kwa shuti kali kutoka nje ya boksi, kabla ya mchezaji wa akiba Gabriel Jesus kufunga bao la nne sekunde chache baada ya kuingia uwanjani.

Watkins alipata bao la kufutia machozi mwishoni mwa mchezo, lakini halikubadilisha taswira ya mchezo ambao Aston Villa walitoka wakiwa vichwa chini.

Kwa upande wa Arteta, huu ulikuwa ushindi wa kuthibitisha kwamba kikosi chake kimevuka hatua ya kuyumba chini ya presha. Arsenal wameonyesha hawategemei mchezaji mmoja na wana uwezo wa kusimama imara hata wanapokosa nyota wao muhimu.

Matokeo ya mechi nyingine zilizopigwa jana EPL

Chelsea 2 vs 2 Bournemouth

Burnley 1 vs 3 Newcastle

Nottingham 0 vs 2 Everton

West Ham 2 vs 2 Brighton

Manchester United 1 vs 1 Wolves

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *