
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amelaani marekebisho ya sheria yaliyopitishwa na Bunge la utawala wa kizayuni wa Israel, Knesset Desemba 29, yanayohusu kusitishwa kwa shughuli za Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA).
Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake Stephane Dujarric, Katibu Mkuu wa UN amesema, marekebisho hayo yanalenga kuzidisha kuzuia uwezo wa UNRWA kufanya kazi na kutekeleza majukumu yake yaliyoidhinishwa.
“Sheria hiyo na marekebisho yake yamekuwa kinyume na hadhi ya UNRWA na mfumo wa kisheria wa kimataifa unaotumika kwa shirika hilo, na yanapaswa kufutwa mara moja,” amesema Katibu Mkuu kupitia taarifa hiyo.
Guterres amesema UNRWA ni sehemu muhimu ya Umoja wa Mataifa, na kwamba Mkataba wa Haki na Kinga za Umoja wa Mataifa unaendelea kutumika kwa UNRWA, mali zake, rasilimali zake, maafisa na wafanyakazi wake.
Wakati huohuo, Kamishna wa Usawa, Maandalizi na Usimamizi wa Migogoro wa Umoja wa Ulaya Hadja Lahbib ameuonya utawala wa kizayuni akisema, mipango yake ya kuzuia mashirika yasiyo ya kiserikali ya kimataifa yasiendeshe shughuli zao za ufikishaji misaada huko Ghaza itakuwa sawa na kuzuia misaada ya kibinadamu inayookoa maisha ya watu.
Katika ujumbe alioweka kwenye mtandao wa kijamii wa X, Lahbib ameeleza bayana: “mipango ya Israeli ya kuzuia mashirika yasiyo ya kiserikali huko Ghaza inamaanisha kuzuia misaada inayookoa maisha. EU imekuwa wazi: sheria ya usajili wa mashirika yasiyo ya kiserikali haiwezi kutekelezwa katika hali yake ya sasa. Vizuizi vyote vya ufikiaji wa kibinadamu lazima viondolewe. IHL (sheria ya kimataifa ya kibinadamu) haiachi nafasi ya shaka: misaada lazima iwafikie wale wanaohitaji”.
Katika upande mwingine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji Maxime Prevot naye pia ameutaka utawala ghasibu wa Israel uondoe vikwazo vya ufikishaji huduma za kibinadamu katika maeneo ya Palestina, akisisitiza kwamba kutoa misaada hakupaswi kuwa “kwa masharti au kisiasa”.
Prevot amekosoa mipango ya utawala wa kizayuni ya kuzuia mashirika yasiyo ya kiserikali ya kimataifa huko Ghaza, akinukuu uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kwamba Israel ina wajibu usio na masharti chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu kuhakikisha utoaji wa misaada kwa raia unafanyika bila kuwekewa vizuizi.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, Siku ya Jumanne, mawaziri wa mambo ya nje wa nchi 10 – ikiwa ni pamoja na Canada, Ufaransa, Japai, na Uingereza – walitoa taarifa ya pamoja wakiitaka Israel ihakikishe mashirika yasiyo ya kiserikali ya kimataifa “yana uwezo wa kufanya kazi Ghaza kwa njia endelevu na inayoweza kutabirika”.
Licha ya makubaliano ya kusitisha vita Ghaza kuanza kutekelezwa tangu mwezi Oktoba, utawala wa kizayuni umeendelea kuvifunga vivuko vya kuingilia eneo hilo, ukizuia kuingizwa nyumba zinazohamishika na vifaa vya ujenzi na hivyo kuzidisha maafa ya kibinadamu yanayowaaathiri zaidi ya Wapalestina milioni mbili wanaoteseka kwa njaa na kuishi kwenye mazingira magumu mno.
Kwa mujibu wa duru za Palestina, watu wasiopungua 414 wameuliwa shahidi na jeshi la utawala wa kizayuni huko Ghaza tangu usitishaji vita ulipoanza kutekelezwa katika eneo hilo lililowekewa mzingiro…/