
Jeshi la Sudan SAF limetangaza kuwa siku ya Jumatano lilirejesha udhibiti wa miji ya Kazgeil na Riyadh iliyoko kwenye jimbo la Kordofan Kaskazini baada ya mapigano na kundi la RSF.
Kwa mujibu wa duru za SAF, vikosi vya jeshi hilo vilifanikiwa kudhibiti maeneo hayo mawili kufuatia mapigano makali, na kuwalazimisha wapiganaji wa RSF kurudi nyuma baada ya kupata hasara za wanajeshi na vifaa.
Video zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na wanajeshi wa Sudan zimeonyesha vikosi vyao vikiwa ndani ya Kazgeil, vikithibitisha kudhibiti eneo hilo lililoko karibu kilomita 45 kusini mwa Al Obeid, mji mkuu wa Kordofan Kaskazini.
Hadi sasa, hakuna kauli rasmi iliyotolewa jeshi lenyewe la Sudan wala RSF.
Kazgeil na Riyadh zilikuwa chini ya udhibiti wa RSF kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu kabla ya jeshi kuzishikilia kwa muda mfupi mwezi Julai, lakini baadaye kundi hilo la waasi lilirejesha udhibiti wake mwishoni mwa mwezi huo.
Majimbo matatu ya Kordofan — Kaskazini, Magharibi na Kusini — yameshuhudia wiki kadhaa za mapigano makali kati ya jeshi la Sudan na RSF, hali iliyosababisha makumi ya maelfu ya watu kuyahama makazi yao.
Kati ya majimbo 18 ya Sudan, RSF inadhibiti majimbo yote matano ya eneo la Darfur magharibi mwa nchi, isipokuwa baadhi ya maeneo ya kaskazini mwa Darfur Kaskazini ambayo bado yako chini ya udhibiti wa jeshi.
Kwa upande wake, jeshi linadhibiti maeneo mengi ya majimbo 13 yaliyosalia kusini, kaskazini, mashariki na katikati mwa nchi, ukiwemo mji mkuu, Khartoum.
Mgogoro kati ya jeshi la Sudan na RSF, ulioanza Aprili 2023, umeshaua maelfu ya watu na kuwafanya mamilioni wengine walazimike kuyahama makazi yao…/