Colombia. Licha ya kuwa wapenzi kwa miaka zaidi ya 10, bado Malkia wa Muziki wa Kilatini kutokea Colombia, Shakira anamdai aliyekuwa mpenzi wake, Gerard Pique miaka 40 ya kuishi pamoja kama ilivyokuwa ndoto yake katika uhusiano huo.

Wawili hao ambao hawakufunga ndoa katika kipindi chote walichodumu, walitangaza kuachana Juni 2022 kutokana na kukosekana kwa uaminifu, huku wakiwa tayari wamejaliwa watoto wawili, Milan (2013) na Sasha (2015).

“Tunasikitika kuthibitisha kwamba tunatengana. Tunaomba faragha kwa wakati huu kwa ustawi wa watoto wetu ambao ndio kipaumbele chetu.” Ilieleza taarifa ikiwa ni muda mfupi baada ya Pique kuhusishwa kutoka na mwanamitindo, Clara Chia.

Utakumbuka Shakira, 48, na Pique, 38, walikutana kwa mara ya kwanza mwaka 2010 huko Madrid, Hispania wakati wakitayarisha video ya wimbo maalamu wa Kombe la Dunia 2010, Waka Waka (This Time for Africa).

Kipindi hicho tayari Pique alikuwa mchezaji wa klabu ya FC Barcelona na timu ya taifa ya Hispania iliyoshinda Kombe la Dunia 2010 huko nchini Afrika Kusini, michuano ambayo Shakira alitumbuiza katika sherehe za ufunguzi kupitia wimbo wake rasmi wa michuano hiyo wa Waka Waka (This Time for Africa).

Akizungumza na Sunday Times, Shakira alidai alilazimika kusimama kazi yake ya muziki kwa miaka mingi kwa sababu ya Pique, mshindi wa Ligi Kuu Hispania (La Liga) mara nane na Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA) mara tatu.

“Kwa muda mrefu nilisimamisha kazi yangu ili kuwa karibu na Pique ili aweze kucheza kandanda. Kulikuwa kujitolea kwa upendo wa hali ya juu,” alisema staa huyo wa kibao cha Hips Don’t Lie (2005).

Hata hivyo, hii sio mara ya kwanza kwa Shakira kutoa kauli inayoonyesha alijitoa sana kwa Pique, katika mahojiano yake na Billboard mwaka uliopita, alisema aliamini kuwa wangeishi pamoja hadi kifo kitakapowatenganisha.

“Kipaumbele changu kilikuwa nyumbani kwangu, familia yangu. Niliamini katika kuishi pamoja hadi kifo kitakapotutenganisha. Niliamini ndoto hiyo. Ndicho nilichotaka kwa ajili yangu na watoto wangu, lakini haikufanikiwa,” alisema.

“Wazazi wangu wamekuwa pamoja, nadhani kwa miaka 50, na wanapendana kama siku ya kwanza, kwa upendo wa kipekee na usioweza kuwa na mbadala. Kwa hiyo najua inawezekana,” alisema Shakira mnamo Septemba 2023.

Ikiwa Shakira anatazama ndoa ya wazazi wake iliyodumu kwa miaka 50 kama mfano bora, basi anamdai Pique miaka 40 ya kuishi pamoja ili kutimiza ndoto yake. Kumbuka wawili hao walitangaza kuwa pamoja Machi 2011 hadi Juni 2022, hivyo walidumu kwa miaka 10 hivi. 

Ikumbukwe uhusiano mwingine wa Shakira na mtoto wa aliyekuwa Rais wa Argentina, Fernando de la Rua, Antonio nao ulidumu kwa miaka 10, kuanzia 2000 hadi Januari 2011 ilipotoka taarifa rasmi ya kuachana kwa kile walichotaja ni uamuzi wa pande zote.

Katika mahojiano na Elle mnamo Septemba 2022, Shakira alizungumza kwa mara ya kwanza kuhusu kuachana kwake na Pique na kusema wamejaribu kuweka mambo sawa kati yao kwa ajili ya watoto wao.

“Bila kujali jinsi mambo yalivyoisha au jinsi mimi na Pique tunavyohisi, yeye ndiye baba wa watoto wangu. Tuna kazi ya kufanya kwa ajili ya watoto hawa na nina imani kwamba tutajua ni kipi bora kwa maisha yao ya baadaye na ndoto zao maishani,” alisema. 

Hata hivyo, akiongea na The Tonight Show With Jimmy Fallon hapo Machi 2023, Shakira alidai hadi kutengana kwao alikuwa amevumilia ujinga mwingi, licha ya uchungu wake, bado Pique haombi msamaha kutokana na matendo hayo. 

Aprili 2023 Shakira aliondoka Barcelona, Hispania na watoto wake, ilidaiwa nyumba aliyokuwa akiishi ni ya Pique na kwamba baba mkwe wake, Joan Pique alimpa notisi kupitia barua pepe akimtaka aondoke au alipe kodi kama mpangaji.

Kupitia mitandao ya kijamii, Shakira alituma ujumbe akiwaaga mashabiki wake wa Barcelona na kusema yeye na wanae wanaanza ukurasa mpya wa kutafuta furaha yao katika kona nyingine ya dunia karibu na familia, marafiki na bahari.

“Nashukuru kwa kila mtu ambaye alinitia moyo, kunifuta machozi yangu na kunifanya nikue. Shukrani kwa hadhira yangu ya Kihispania ambayo daima imenifunika kwa upendo na uaminifu wao,” alisema Shakira ambaye alitimkia Miami, Marekani.

Na katika muziki, Shakira aliyeanza kufanya kazi na Sony Music Colombia akiwa na umri wa miaka 13, tayari ameuza rekodi milioni 80 dunini kote na kushinda tuzo tatu za Grammy, tuzo 12 za Latin Grammy, tuzo nne za MTV na tuzo 39 za Billboard Latin Music.

Baada ya Michael Jackson na Eminem, Shakira ndiye anafuata kama msanii wa tatu kuwa na nyimbo nne kutoka miongo tofauti kufikisha wasikilizaji (streams) zaidi ya milioni 100 kwenye mtando wa Spotify ambao mwaka 2018 ulimtaja kama msanii wa Kilatini aliyesikilizwa zaidi katika jukwaa hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *