Kiungo wa zamani wa England, Steven Gerrard amesema kuwa kilichofanya kizazi chake katika timu ya taifa ya nchi hiyo kushindwa kutamba katika mashindano tofauti ni ujivuni ambao haukuwa na faida.

Gerrard alikitumikia kikosi cha England kilichokuwa na wachezaji wengi wenye majina makubwa hadi kikapewa jina la ‘Kizazi cha Dhahabu’ ambacho kwa nyakati tofauti kilifundishwa na makocha Sven-Goran Eriksson, Steve McClaren, Fabio Capelo na Roy Hudgson.

Hata mafanikio makubwa ya kikosi hicho yalikuwa ni kuishia hatua ya robo fainali katika Fainali za Kombe la Dunia na Fainali za Ulaya na haikusogea juu ya hapo.

Lakini kizazi cha sasa kimefanikiwa kutinga nusu fainali ya Kombe la Dunia mara mbili huku ikifika fainali mbili mfululizo za Kombe la Ulaya.

Na Gerrard anaamini kwamba kizazi chake kingeweza kufanya vizuri kama wachezaji wasingekuwa wabinafsi na wenye kujiona kila mmoja ni zaidi ya mwenzake.

“Kulikuwa na tatizo kubwa ndani ya England kwa maoni yangu. Nafikiri wote tulikuwa wajivuni wa kushindwa.  Natazama sasa naona Carragher amekaa pembeni ya Paul Scholes na wanaonekana kama walikuwa timu moja kwa miaka 20.

“Naona uhusiano wa Carragher na Gary Neville na wanaonekana kama walikuwa timu moja kwa miaka20.

“Sasa kwa nini hatukuunganika wakati tulipokuwa na miaka 20, 21, 22, 23? Ilikuwa ni ubinafsi? Ilikuwa ni uhasama? Kwa nini tumepevuka vya kutosha sasa. Kwani nini hatukuunganika wakati tulipokuwa wachezaji katika kikosi cha England?

“Hatukuwa marafiki au tumeunganika. Hatukuwa timu. Hatukuwahi katika shindano lolote kuwa timu nzuri na imara,” amesema Gerrard.

Gerrard anasema kila mchezaji alijiona yeye ni zaidi ya mwingine.

“Ilikuwa ni kama sijihisi kuwa sehemu ya timu. Sikujisikia kuunganika na wachezaji wenzangu wa England,” amesema Gerrard.

Gerrard amesema kuwa mambo hayakuwa hivyo pindi alipokuwa kati kikosi cha Liverpool kwani alipewa sapoti kubwa pindi alipokuwa na jezi ya timu hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *