Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Cecilia Paresso amewaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025 kwenda kumpigia kura mgombea urais kupitia chama hicho, Samia Suluhu Hassan kwa kuwa anatosha.

Paresso aliyewahi kuwa mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Arusha, ameyasema hayo katika mikutano ya kampeni za mgombea mwenza wa urais wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi iliyofanyika leo Jumatano, Oktoba 8, 2025 katika visiwa vya Pemba na Unguja.

Kada huyo ambaye ni miongoni mwa wanaounda timu ya Dk Nchimbi aliyetua Zanzibar kusaka ushindi wa Samia wa urais wa Tanzania, Dk Hussein Mwinyi wa Zanzibar, wabunge na wawakilishi.

“Tunatambua huu ni mwaka wa uchaguzi, CCM kimetuletea viongozi wenye sifa za kipekee na kwenye nafasi ya urais, imetuletea mwana mama mzalendo, mpambanaji na shupavu kwelikweli.

“Chama kimemleta ili tumchague kwa kumpigia kura. Katika kazi kubwa aliyoifanya kwa miaka minne na nusu ni udhibitisho kuwa anatosha na kina mama tuna jambo letu Oktoba 29,” amesema Paresso na kuongeza:

“Tukampigie kura za kishindo na za heshima. Kina baba na vijana nanyi twendeni tukapige kura kwa Samia, Dk Mwinyi, wabunge na madiwani wote ili kwa pamoja hii timu ikatuletee maendeleo.”

Pia, Pareso amewaomba Wazanzibar kumwamini tena Dk Mwinyi kwani amefanya kazi kubwa kama iliyofanywa na Rais Samia: “Kazi iwe moja tu kuwachagua tena waendelee kutuongoza.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *