KIPA kijana wa Kitanzania, Abdallah Hamisi anaendelea kuandika rekodi yake kimyakimya katika Ligi Kuu ya Falme za Kiarabu (UAE Pro League) baada ya kupandishwa kutoka kikosi cha vijana hadi timu ya wakubwa msimu huu.

Abdallah ambaye yupo Abu Dhabi, sasa anacheza kikosi cha U23 kama kipa namba moja huku akiwa kipa wa nne katika timu ya wakubwa, hatua inayotajwa kuwa ni kubwa kwa maendeleo yake.

Kwa mujibu wa meneja wake, Mansour Alawi kipa huyo alijiunga na klabu hiyo mwaka 2022 na tangu hapo amekuwa akipanda ngazi taratibu hadi kufikia hatua ya kupandishwa rasmi mwaka huu.

Akizungumza na Mwanaspoti meneja huyo amesema: “Ameonyesha kiwango cha kuongezeka kila siku, ndiyo maana makocha wakaona anastahili nafasi kwenye timu ya wakubwa,” amesema Mansour.

Takwimu zinaonyesha hadi sasa amecheza mechi nane za U23 na kufanikiwa kuondoka na clean sheet tano, rekodi inayomfanya aongoze miongoni mwa makipa wa kikosi hicho.

Mbali na hapo, alipata nafasi ya kucheza mechi mbili za timu ya wakubwa katika maandalizi ya msimu (pre-season) yaliyofanyika Morocco, jambo lililoendelea kumpa uzoefu mkubwa wa kimataifa.

Safari yake ilianzia hapa nyumbani alipokuwa sehemu ya timu ya taifa ya U17 kabla ya kuondoka kwenda Falme za Kiarabu. Katika hatua za makuzi, aliwahi kucheza Fair Play Academy, kisha Sahare All Stars kama kipa wa U15, baadaye akatua Simba U17.

Baadaye akaenda African Sports ya Daraja la Kwanza ambako ndiko alikopata nafasi ya majaribio yaliyompeleka hadi UAE.

Mansour aliongeza wakati wanampeleka majaribio waliona kitu kikubwa ndani ya ndoto za kijana huyo. “Tuliona eneo sahihi kwa maslahi ya taifa letu na maendeleo yake binafsi, tukachukua uamuzi wa kutimiza malengo yake,” amesema meneja huyo akisisitiza kuwa ni mradi waliouanza miaka saba iliyopita wa kuwaandaa makipa.

Meneja huyo anafichua kuwa Abdallah pia aliwahi kwenda kufanya majaribio katika klabu ya Granada CF nchini Hispania, ambako mambo yalielezwa kwenda vizuri.

“Upo uwezekano siku zijazo akaonekana katika moja ya ligi tano bora barani Ulaya kama mambo yataenda kama tunavyotarajia. Kwa sasa tunasubiri majibu baada ya majaribio kukamilika.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *