
Ndani ya ukimbi wa Baraza la Kiuchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa ECOSOC wajumbe 193 wa Umoja wa Mataifa wamesheheni kuadhimisha tukio hili muhimu. Akitoa taarifa yake katika hafla hiy Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, hakutafuna maneno wala kuficha hali halisi inayoikabili dunia hivi sasa
Anasema “Licha ya dalili za maendeleo ya kweli, dunia yetu iko katika hali tete.”
Amewasilisha taswira nzito, migogoro ikiendelea kuenea huku matumizi ya kijeshi yakipanda kwa kasi, ukosefu wa usawa ukiongezeka, wakati ufadhili wa maendeleo ukizidi kuporomoka, na suluhu za mabadiliko ya tabianchi zinasonga polepole wakati joto la dunia likiendelea kupanda. Guterres amesisitiza
“Migogoro hii iliyounganishwa haiwezi kutatuliwa kwa mbinu za upande mmoja au kwa nguvu za kijeshi pekee. Inahitaji hatua za haraka na za pamoja.”
Kwa miongo minane sasa, ECOSOC imekuwa mhimili wa maendeleo ya kimataifa kuanzia Azimio la Ulimwengu la Haki za Binadamu hadi Malengo ya Maendeleo Endelevu SDG,s huku ikipanua wigo wa ushiriki wa asasi za kiraia, na sasa zaidi ya mashirika yasiyo ya kiserikali 6,500 yameidhinishwa kushiriki rasmi katika kazi zake.
Lakini Katibu Mkuu ameonya kuwa mafanikio ya zamani pekee hayatoshi kuisukuma dunia mbele.
Amezihimiza nchi wanachama kuchukua hatua za haraka kutekeleza mageuzi waliyokubaliana katika Mkataba wa Zama Zijazo ikiwemo kuifanyia marekebisho mifumo ya kifedha ya kimataifa ili izihudumie vyema zaidi nchi zinazoendelea.
Hii inamaanisha kuongeza uwezo wa kukopesha wa benki za maendeleo ya kimataifa, kupunguza mzigo mkubwa wa madeni, na kutoa nafasi ya haki zaidi kwa nchi zinazoendelea katika taasisi za kifedha za dunia.
“ECOSOC ina jukumu muhimu sana katika dunia yetu iliyogawanyika na yenye ukosefu wa usawa na hatuna muda wa kupoteza katika kuliimarisha.
Wakati Umoja wa Mataifa ukiadhimisha miaka 80 tangu kikao cha kwanza cha ECOSOC, Guterres amewakumbusha wajumbe kuwa maendeleo hayaji mara moja lakini kuchelewa hakukubaliki tena.
“Wajibu wetu ni kusonga mbele kwa kasi kadri tuwezavyo kwa ajili ya watu wanaotutegemea na kwa uthabiti unaohitajika ili tufanye mambo kwa usahihi.”
Katika dunia iliyogawanyika na inayotafuta mwelekeo, ujumbe wa Katibu Mkuu uko bayana, ushirikiano wa kimataifa si jambo la historia bali ni hitaji la lazima kwa mustakabali wa dunia.