Akizungumza katika mahojiano maalum na Idhaa ya Umoja wa Mataifa, Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia na AI katika Elimu wa UNESCO, Shafika Isaacs, amesema kuna dhana potofu tatu kubwa zinazoongoza mjadala wa AI katika elimu, ambazo zinaweza kuathiri mustakabali wa ujifunzaji kwa haki na usawa.

Dhana potofu ya kwanza ni ile ya AI kuchukua nafasi ya mwalimu, ambapo UNESCO inasema hilo ni kosa la msingi katika uelewa wa elimu.

“Kwa hivyo kama UNESCO, tunaamini kwamba hili ni kosa la msingi. AI inaweza kudhibiti uhamishaji wa taarifa, lakini haiwezi kudhibiti maendeleo ya binadamu. Elimu kimsingi ni uzoefu wa kijamii, kibinadamu na kitamaduni, si upakuaji wa taarifa kiufundi.”

Imani potofu ya pili ni kile kinachoitwa personalised learning, ambapo mara nyingi mwanafunzi huachwa peke yake mbele ya kompyuta, akiongozwa na algorithm, badala ya ujifunzaji wa kijamii unaokuza fikra pevu na ubunifu.

Imani potofu ya tatu ni dhana kwamba kujifunza kwa haraka ni kujifunza vizuri, ilhali UNESCO inasisitiza kuwa elimu inahitaji muda na kufikiri kwa kina.

Pamoja na hilo, UNESCO inaonya kuhusu hatari tatu kubwa endapo AI itatumika bila mwelekeo wa kibinadamu.

Hatari ya kwanza ni wanafunzi kuruhusu AI kufanya kazi yote ya kufikiri kwa niaba yao.

“Kwahiyo, tunahatarisha kuwa na kizazi ambacho ni wavivu wa utambuzi, na ufasaha katika kuandika, lakini ambacho hakiwezi kufikiria kwa kina, kwa kutafakari, na kwa umakini. Na hiyo ni hatari kubwa.”

Hatari ya pili ni kuongezeka kwa upendeleo wa mifumo ya algorithm na kupotea kwa udhibiti wa taarifa na takwimu za wanafunzi, huku ya tatu ikiwa ni mmomonyoko wa mkataba wa kijamii wa elimu pale mwalimu anapopunguzwa kuwa msimamizi wa taarifa.

Kwa msimamo wake, UNESCO inahitimisha kuwa lengo si kujenga madarasa yenye teknolojia nyingi zaidi, bali kuhakikisha AI inatumika kuimarisha elimu inayozingatia utu wa binadamu, haki, usawa na ujifunzaji wenye maana kwa wote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *