
Dar es Salaam. Benki ya Stanbic Tanzania imeendelea kuonyesha umuhimu wa masoko ya mitaji katika kuchochea maendeleo ya muda mrefu ya nchi baada ya kushiriki kama Mratibu Mkuu wa Hatifungani ya Makazi iliyotolewa na kampuni ya First Housing Finance Tanzania (FHF).
Hatifungani hiyo inalenga kuhamasisha mtaji wa ndani kwa ajili ya kugharamia mikopo ya nyumba, hatua inayotarajiwa kuongeza upatikanaji wa makazi nafuu na kuchochea shughuli za kiuchumi hususan katika sekta ya ujenzi.
FHF ni miongoni mwa taasisi zinazoongoza nchini katika utoaji wa mikopo ya nyumba nje ya mfumo wa benki za kawaida. Kufikia Machi 31, 2025, kampuni hiyo ilikuwa na asilimia 5.3 ya soko la mikopo ya nyumba, ikiwa tayari imetoa mikopo yenye thamani ya Sh36 bilioni kwa mamia ya wanufaika.
Toleo la kwanza la hatifungani hiyo lina thamani ya Sh5 bilioni, huku kukiwa na uwezekano wa kuongeza hadi Sh3 bilioni zaidi kupitia utaratibu wa greenshoe option, hatua inayoashiria kuimarika kwa imani ya wawekezaji katika vyombo vya kifedha vinavyochanganya faida na matokeo chanya kwa jamii.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa hatifungani hiyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Stanbic Bank Tanzania, Manzi Rwegasira, alisema sekta ya makazi ina nafasi kubwa katika ustawi wa taifa.
“Makazi siyo tu sehemu ya kuishi, bali ni msingi wa familia imara, jamii zenye nguvu na ukuaji endelevu wa uchumi. Masoko ya mitaji yanaweza kuwa nyenzo muhimu katika kushughulikia mahitaji halisi ya wananchi,” alisema Rwegasira.
Kwa mujibu wa benki hiyo, fedha zitakazopatikana kupitia hatifungani hiyo zitaiwezesha FHF kupanua utoaji wa mikopo ya nyumba kwa wananchi wengi zaidi, hatua itakayochochea ajira katika sekta ya ujenzi pamoja na minyororo ya ugavi inayohusiana na sekta hiyo.
Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Kibenki kwa Makampuni na Uwekezaji wa Stanbic, Ester Manase, alisema uwazi na nidhamu katika uundaji wa vyombo vya kifedha ni msingi wa kuvutia wawekezaji na kukuza masoko ya mitaji ya ndani.
“Ili masoko ya mitaji yakue kwa kasi, ni lazima vyombo vinavyotolewa viwe vya uwazi, vinavyoaminika na vinavyoendana na malengo ya kiuchumi ya muda mrefu. Hatifungani ya Makazi ni mfano wa jinsi mtaji wa sekta binafsi unavyoweza kusaidia maendeleo kwa uwajibikaji,” alisema Manase.
Naye Makamu Mkuu wa Rais wa Kitengo cha Soko la Mitaji na Usambazaji wa Madeni wa Stanbic, Sarah Mkiramweni, alisema mpango huo unaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga ukuaji jumuishi na ustawi wa jamii.
“Fedha za makazi zina mchango mkubwa katika maendeleo ya miji, utulivu wa familia na tija ya muda mrefu ya uchumi,” alisema.
Stanbic imewahimiza wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kushiriki katika hatifungani hiyo, ikieleza kuwa ni fursa ya kupata faida za kifedha huku wakichangia kuboresha maisha ya Watanzania kupitia upatikanaji wa makazi.
Benki hiyo imeeleza kuwa itaendelea kubuni suluhisho za kifedha zinazounganisha uwekezaji na maendeleo ya kijamii, ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika kuimarisha sekta ya fedha na uchumi wa Tanzania kwa ujumla.