“Nilivuliwa nguo bila hiari yangu na Grok ya Elon Musk kwenye X,” Naibu Waziri Mkuu wa Sweden, Ebba Busch, alisema katika video ya hivi karibuni kwenye jukwaa hilo. Yeye ni mmoja wa waathiriwa wengi wa kipengele cha roboti ya Akili Mnemba ya X, Grok, kinachowaruhusu watumiaji kuwaondolea wanawake na watoto mavazi yao kidijitali. Katika kipindi cha chini ya wiki mbili, Grok ilizalisha picha milioni tatu za kingono, zikiwemo makumi ya maelfu zinazoonekana kuwa zinawaonyesha watoto.
Sasa, Tume ya Ulaya, chombo cha utendaji cha Umoja wa Ulaya (EU), imeanzisha uchunguzi dhidi ya Grok chini ya Sheria ya Huduma za Kidijitali (Digital Services Act – DSA). Tume hiyo ilisema itafanya “tathmini iwapo kampuni ya mtandao wa kijamii X ilitambua ipasavyo na kupunguza hatari zinazohusiana na kuanzishwa kwa uwezo wa Grok ndani ya X katika Umoja wa Ulaya.”
Uchunguzi huo unaweza kuweka mfano muhimu katika kukabiliana na makampuni ya teknolojia ya Marekani na kulinda raia dhidi ya ukiukwaji wa faragha. “Kama wanaweza kumkabili Musk, hilo ni jambo kubwa,” alisema Joanna Bryson, profesa wa maadili na teknolojia katika Chuo Kikuu cha Hertie mjini Berlin, katika mazungmzo na DW. “Inawaonyesha wote kuwa EU iko makini.”
EU ina sheria za ulinzi dhidi ya madhara ya AI
Lakini EU ina nguvu kiasi gani? Chini ya sheria zake, umoja huo unaweza kudhibiti huduma za kidijitali kwa namna sawa na bidhaa halisi. Kama vile vinyago au vifaa visivyo salama vinavyoweza kupigwa marufuku sokoni Ulaya, majukwaa ya mtandaoni yanayokiuka sheria za EU yanaweza kulazimishwa kubadilika — au hata kuzuiwa kabisa kufanya kazi ndani ya EU.
“DSA bila shaka ni kanuni yenye nguvu zaidi duniani ya kudhibiti majukwaa,” alisema Philipp Hacker, profesa wa sheria na maadili katika Chuo Kikuu cha Viadrina mjini Frankfurt an der Oder. Badala ya kulenga teknolojia mahususi, sheria hiyo inashughulikia makundi mapana kama vile “hatari za kimfumo,” jambo linaloipa Tume ya Ulaya unyumbufu wa kujibu madhara mapya kadri AI inavyoendelea kukua. Kipengele cha Grok cha “kuvua nguo” hakikuwepo wakati DSA ilipoanza kutumika mwaka 2022.
EU ina zana kuu mbili za utekelezaji. Inaweza kuitoza X faini ya hadi asilimia 6 ya mapato yake ya kila mwaka duniani kote — hatua ambayo tayari ilichukuliwa Desemba, ilipolitoza jukwaa hilo faini ya euro milioni 120 (dola milioni 143) kwa kukiuka sheria za uwazi za DSA. Katika kesi za ukiukwaji wa mara kwa mara, Tume pia inaweza kulizuia kabisa jukwaa hilo ndani ya EU. Kwa sasa, kutozwa faini kunatazamwa kama hatua inayowezekana zaidi.
Nguvu ya EU inaongezwa na ukubwa wa soko lake. Kama mojawapo ya masoko makubwa zaidi ya watumiaji duniani, lina ushawishi mkubwa juu ya makampuni ya teknolojia ya kimataifa.
EU yachelewesha kuanza kwa uchunguzi wa Grok
Hata hivyo, wataalamu wanahoji kama Tume itasukuma vya kutosha kuweka mfano wa kudumu. “Tuna masharti mengi yanayolinda haki za msingi. Tatizo ni utekelezaji wake, kuhakikisha hayapuuzwi,” anasema Marco Bassini, mhadhiri msaidizi wa Haki za Msingi na Akili Mnemba katika Chuo Kikuu cha Tilburg.
Katika kipindi ambacho mahusiano ya EU na Marekani yako chini ya msukosuko, Brussels imekuwa mwangalifu kutumia kikamilifu nguvu zake za udhibiti dhidi ya makampuni ya teknolojia ya Marekani. Kulingana na ripoti ya gazeti la Kijerumani la Handelsblatt, kuanzishwa kwa uchunguzi wa Grok kulicheleweshwa na ofisi ya Rais wa Tume ya Ulaya, Ursula von der Leyen, katikati ya mvutano wa ushuru kati ya EU na Marekani kuhusu Greenland. Hapo awali, Waziri wa Biashara wa Marekani, Howard Lutnick, aliwahi kuhusisha upunguzaji wa ushuru na kulegezwa kwa kanuni za teknolojia za EU.
“Nadhani kosa kubwa lilifanywa,” alisema Mbunge wa Bunge la Ulaya (MEP) Alexandra Geese alipozungumza na DW. “Kulikuwa na hofu kubwa kuhusu mwitikio wa utawala wa Marekani.”
Wataalamu wana shaka EU itakwenda mbali kiasi gani
Ingawa kuanzishwa kwa uchunguzi hatimaye kunatazamwa kama ishara chanya, mashaka bado yapo kuhusu ni kwa kiasi gani Tume iko tayari kwenda. “Mtu laazima atofautishe kati ya msimamo wa kisheria na msimamo wa kijiografia wa kisiasa,” alisema Bryson. “Tume huangalia yote mawili.”
Pia kuna mashaka iwapo faini ya asilimia 6 itatosha kubadili mwenendo wa mtu tajiri zaidi duniani. “Tunapaswa kuongeza kiwango hiki ili makampuni yaanze kuzingatia kwa umakini kile ambacho wabunge wanatarajia barani Ulaya,” MEP Axel Voss aliiambia DW.
Hakuna ratiba maalum ya uchunguzi huo. Kulingana na wataalamu, inaweza kuchukua miezi kadhaa kabla ya Tume kufikia hitimisho.
