Marekani imezindua mradi huo wa upanuzi wa uwanja wa ndege katika kambi ya kijeshi iliyo karibu na mpaka wa Kenya na Somalia, ujenzi huo unalenga kuimarisha shughuli za kupambana na ugaidi katika eneo la Pembe ya Afrika.
Kambi ya jeshi la anga huko Manda Bay ni eneo la Jeshi la Ulinzi la Kenya katika Kaunti ya Lamu linalotumiwa na vikosi vya Marekani na kwa muda mrefu imekuwa kitovu cha kimkakati katika mapambano dhidi ya kundi la itikadi kali la Al-Shabaab lenye mahusiano na Kundi la kigaidi la Al-Qaeda.
Mnamo mwaka 2024, rais wa zamani wa Marekani Joe Biden alitangaza mipango ya kuifanya Kenya kuwa mshirika mkuu wa kwanza asiye mwanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO katika eneo Afrika la Kusini mwa Jangwa la Sahara, na akaongeza uhusiano wa kijeshi na wa kidiplomasia, ingawa haukuwepo mkataba rasmi wa usalama uliotiwa saini.
Kwenye uzinduzi wa ujenzi huo siku ya Alhamis, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Christopher Landau alisema kituo hicho cha ulinzi kinawakilisha ahadi inayoonekana wazi, ambayo ni ulinzi wa pamoja kati ya Marekani na Kenya.
Mnamo mwaka 2020, raia watatu wa Marekani waliuawa wakati wapiganaji wa Al-Shabaab walipofaulu kuvuka ulinzi mkali katika Kambi ya Simba, ambayo ni sehemu ya kambi ya kijeshi ya Ghuba ya Manda, na waliharibu ndege kadhaa pamoja na magari ya kijeshi.
Itakumbukwa mnamo mwaka 1998, balozi za Marekani nchini Kenya na Tanzania zililengwa kwa wakati mmoja na wapiganaji wa Kundi la Al-Qaeda. Mashambulizi hayo yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 200, wakiwemo Wamarekani 12, na maelfu ya watu walijeruhiwa.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Christopher Landau, katika uzinduzi wa upanuzi wa uwanja wa ndege kwenye kambi ya kijeshi katika ghuba ya Manda pia aliipongeza Kenya kwa mchango wake kwenye vikosi vya kimataifa katika kuleta utulivu nchini Haiti. Amesema Kenya ni mshirika muhimu sana katika hilo,na katika misheni hiyo na pia katika kusaidia kupanga kikosi kipya cha kuyaangamiza magenge.
Taifa hilo la Afrika Mashariki linaongoza ujumbe unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, ambao unalenga kuwasaidia polisi wa taifa la Haiti kukabiliana na magenge yanayodhibiti sehemu kubwa za nchi hiyo.