Maafisa 15 wa Iran wawekewa vikwazo na Umoja wa UlayaMaafisa 15 wa Iran wawekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya

Mashirika sita ya Iran zikiwemo bodi zinazohusika na uangalizi wa maudhui ya mtandaoni, pia zilijumuishwa katika orodha ya waliowekewa vikwazo. Makamanda wa juu wa kikosi maalum cha walinzi mapinduzi Iran, IRGC ni miongoni pia mwa waliowekewa vikwazo na Umoja huo.

Uamuzi huo wa nchi wanachama 27 wa Umoja wa Ulaya, ni wa hivi karibuni kuchukuliwa na nchi za Magharibi kufuatia ghasia za Iran, zilizosababishwa na maandamano ya kupinga kudorora kwa uchumi wa taifa hilo. Wanaharakati wa ndani na nje ya Iran wanadai kuwa maandamano hayo yaliyogeuka kuwa ya nchi nzima ya kuipinga serikali, yamesababisha mauaji ya waandamanaji 6,300.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas amesema kikosi hicho maalum cha Iran kilikuwa na jukumu maalum la kuwakandamiza waandamanaji na kutokana na hilo kitawekwa katika orodha sawa na makundi ya kigaidi kama Al Qaida, Hamas na Daesh au dola la kiislamu kama linavyojulikana na wengi.

“Tumekubaliana kukiwekea vikwazo kikosi maalum cha walinzi mapinduzi Iran, hii itakiweka katika orodha sawa na al Qaeda, Hamas na Daesh. Ukishiriki matendo ya kigaidi utachukuliwa kama gaidi. Ni wazi, kwamba idadi ya waliouwawa Iran ni kubwa na hatua dhidi ya waandamanaji zilikuwa kali.  Tunatuma ujumbe kwamba ukiwakandamiza watu utawajibishwa kwa kuwekewa vikwazo,” alisema Kaja Kallas.

Indischer Ozean 2012 | USS Abraham Lincoln
Meli ya jeshi la Marekani aina ya USS Abraham Lincoln ikielekea eneo la Mashariki ya Kati ili itumike kuishambulia Iran kutoka baharini. Picha: Eric S. Powell/ABACA/picture alliance

Iran imekuwa ikiikosoa Ulaya kwa hatua yake hiyo ya kukiwekea vikwazo kikosi chake kama ilivyofanya Marekani mwaka 2019. Hatua hiyo ya Umoja wa Ulaya, inaongeza shinikizo la kimataifa kwa Jamhuri hiyo ya kiislamu, wakati ikiwa inakabiliwa na kitisho kikubwa kutoka Marekani cha kuishambulia. Rais Donald Trump awali alisema ataishambulia kijeshi Iran iwapo itaendelea kuwakamata na kuwaua waandamanaji.

Marekani yapeleka meli zake za kivita Mashariki ya Kati

Jeshi la Marekani tayari linasemekana kupeleka meli yake kubwa ya kijeshi aina ya USS Abraham Lincoln na makombora mengine katika eneo la Mashariki ya Kati ili litumike kuishambulia Iran kutoka baharini. Haijawa wazi lakini hadi sasa iwapo Donald Trump atatumia nguvu kubwa kiasi gani dhidi ya Iran.

Iran kwa upande wake imesema itajibu shambulizi la iana yoyote dhidi yake, ikilenga kambi za kijeshi za Marekani na Israel pamoja na mataifa mengine yoyote yatakayowaunga mkono. Iran imetoa onyo kwa meli zilizoko baharini kwamba inapanga kufanya luteka  ya kijeshi wiki ijayo, itakayojumuisha makombora kurushwa katika mlango wa bahari wa Hormuz, hatua itakayosambaratisha asilimia 20 ya biashara za mafuta duniani zinazopitia njia hiyo ya bahari. 

Huku hayo yakiarifiwa maafisa wakuu wa Ulinzi na ujasusi kutoka Israel na Saudi Arabia, wanatarajiwa kusafiri kuelekea Marekani wiki hii, kwa mazungumzo kuhusu Iran. Bado Ikulu ya Marekani haijasema lolote kuhusu ziara ya maafisa hao. Lakini gazeti la Axios limeripoti kuwa maafisa wa Israel wanakwenda kutoa taarifa zao za kijasusi za maeneo ya kulengwa Iran huku Saudi Arabia ikitarajiwa kujaribu kuzuwia mzozo kutanuka katika maeneo mengine ya Mashariki ya Kati.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *