Araqchi Hata hivyo ameonya kuwa nchi yake haitafanya majadiliano yatakayohusisha uwezo wa Iran kujilinda. Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran ametoa kauli hiyo katika mkutano na waandishi wa habari mjini Istanbul  ambako yuko ziarani akiwa sambamba na mwenzake wa Uturuki Hakan Fidan.

Katika mkutano huo aliongeza kuwa, “Ningependa kuweka wazi kabisa kuwa masuala yoyote yanayohusiana na ulinzi wa Iran hayatokuwa sehemu ya majadiliano. Sidhani kama kuna nchi iliyo tayari kuweka rehani ulinzi na usalama wake kwa mtu yeyote. Usalama wa watu wa Iran haumhusu yeyote na tutatunza na kutanua uwezo wetu wa ulinzi kwa namna yoyote ili kuilinda nchi yetu.”

 Zaidi Araqchi ameweka bayana kuwa hadi sasa hakujawa na mipango yoyote ya mazungumzo kati ya Iran na Marekani. Kauli hiyo ya Araqchi imetolewa siku kadhaa baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kutishia kuishambulia Iran kama haitarejea kwenye mazungumzo ya nyuklia na kufikia makubaliano. Akijibu vitisho hivyo Araqchi amesema kuwa Tehran iko tayari kwa vyote iwe vita au mazungumzo.

Juhudi za kikanda kuzuia vita zinaendelea

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya nje wa Uturuki ameeleza kuwa ameshazungumza na Mjumbe maalumu wa Marekani Steve Witkoff na ataendelea kuzungumza na maafisa wa Marekani kuhusu Iran. Pamoja na hayo ameitaka Washington ikatae shinikizo la Israel la kuishambulia Iran akionya kuwa kufanya hivyo kutahatarisha zaidi hali Mashariki ya Kati.

Türkei Istanbul 2026 | Außenminister Hakan Fidan und Abbas Araghchi bei Treffen
Picha: Turkish Foreign Ministry/Handout via REUTERS

Washirika wa kikanda ikiwemo Uturuki, Umoja wa Falme za Kiarabu na Saudi Arabia wamekuwa wakifanya juhudi za kuzuia makabiliano ya kijeshi kati ya nchi hizo mbili.

Mapema Alhamisi, Trump alilegeza msimamo na kusema kuwa anafanya mazungumzo na Iran na kwamba ametoa nafasi ya uwezekano wa kuepuka makabiliano ya kijeshi na taifa hilo. Ametoa kauli hiyo muda mfupi baada ya kutuma manowari ya kivita katika Mashariki ya Kati na kutoa onyo awali kuwa Tehran haina muda tena.

Wakati huohuo, Iran imetangaza kuwa inapanga hatua ya kisasi kwa kuyaweka majeshi ya nchi za Umoja wa Ulaya kwenye orodha ya makundi ya kigaidi. Hayo yanajiri ikiwa ni siku moja tu tangu mawaziri wa  umoja huo walipolijumuisha jeshi la mapinduzi ya Iran kwenye orodha ya makundi ya kigaidi sawa na kundi la Al Qaeda na IS.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *