
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali Youssouf amelaani mashambulizi ya hivi karibuni huko Niger ikiwa ni pamoja na shambulio kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Hamani Diori katika mji mkuu Niamey. Ali Youssouf amesisitiza kwa mara nyingine tena kwamba Umoja wa Afrika uko pamoja na Niger.
Yousouf amesema kuwa amesikitishwa pakubwa na shambulio lililofanywa na watu wenye silaha katika uwanja wa ndege wa Niamey usiku wa tarehe 28 Januari kuamkia tarehe 29 na shambulio jingine lililofanywa Januari 18 mwaka huu katika kijiji cha Bosiye magharibi mwa Niger ambapo raia wasiopungua 30 waliuawa.
“Vitendo hivi vya kikatili ni sehemu ya kampeni ya ugaidi inayofanywa na vikundi vyenye nmisimamo mikali vinavyolenga kwa makusudi raia na miundombinu ya umma,” amesema Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika.
Mahmoud Ali Youssouf pia mepongeza hatua za haraka na kali zilizochukuliwa na askari usalama wa Niger na kusaidia kudhibiti hujuma dhidi ya uwanja wa ndege wa Hamani Diori huko Niamey, mji mkuu wa Niger.
Umoja wa Afrika umebainisha mshikamano wake na wananchi wa Niger na kutoa mkono wa pole kwa familia za wahanga na kwa serikali ya Niger.
Youssouf amekiri kuhusu juhudi za mamlaka husika za Niger za kupambana na ugaidi na misimamo mikali, na kuashiria operesheni za jeshi la nchi hiyo dhidi ya wanamgambo wenye silaha.
Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika kwa mara nyingine tena amesisitiza kuwa ugaidi na misimamo mikali ya kufurutu ada ni tishio kubwa kwa amani, utulivu na mamlaka ya kjitawala nchi katika nchi zilizokumbwa na ugaidi na kusema Tume ya Umoja wa Afrika iko tayari kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali ya Niger za kupambana na ugaidi na misimamo mikali.