ACHANA na matokeo ya ugenini dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika, kocha wa zamani wa Yanga, Sead Ramovic amefichua siri inayombeba Uarabuni.
Kocha huyo aliyeinoa Yanga kwa kipindi kifupi akitokea TS Galaxy ya Sauzi, amesema kuna tofauti ya kushangaza kati ya ukocha Afrika Kusini na Algeria, aliko kwa sasa akiinoa CR Belouizdad iliyoshinda jioni ya leo Jumapili kwa mabao 3-0 ikiwa ugenini.
Kocha huyo Mjerumani alitumia miaka mitatu katika klabu ya TS Galaxy iliyopo Ligi Kuu ya Afrika Kusini, ambapo alisifiwa sana kwa kuifanya klabu ibaki na ushindani licha ya kuwa na bajeti ndogo sana.
Aliifikisha fainali ya Carling Knockout 2023, japo ilipoteza kwa mikwaju ya penalti dhidi ya Stellenbosch.
Pia, licha ya klabu kupigwa marufuku ya usajili na FIFA na kulazimika kuuza wachezaji wake bora mara kwa mara, Ramovic aliendelea kuiweka timu katika kiwango kizuri katika Ligi.
Ramovic (46) aliondoka TS Galaxy Novemba 2024 kutafuta changamoto mpya kwa kujiunga na akiwa Yanga ya Tanzania na baada ya kukaa kwa muda mfupi, aliteuliwa kuwa kocha wa CR Belouizdad ya Algeria Februari mwaka jana.
Akiwa.amebakiwa na mechi 11 tu ili awe kocha aliyehudumu muda mrefu zaidi katika historia ya klabu ya CR Belouizdad.
Ramovic amekiri kwamba maisha ya ukocha Algeria ni magumu zaidi, akieleza tofauti kati ya huko na Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL).
“Tofauti iko wazi: ubora wa wachezaji, kiwango cha ushindani na presha. Algeria kila timu ni ngumu kucheza nayo. Wanawekeza sana na matarajio ni makubwa kupita kiasi,” amesema Ramovic na kuongeza;
“Nilipokuwa TS Galaxy, presha haikuwa kubwa hivyo. Ukimaliza nafasi ya tano, ya sita au hata ya kumi, ilikuwa sawa. Lengo kuu lilikuwa kukuza wachezaji ambao klabu inaweza kuwauza, na nadhani tulifanya kazi nzuri sana.”
“Lakini kushinda mataji katika mazingira kama hayo ni ngumu sana kwa sababu kila msimu unapoteza wachezaji saba au wanane.”
“Tofauti na klabu zenye fedha nyingi, huwezi tu kununua wachezaji kwa mamilioni. Unalazimika kutegemea akademi yako. Hilo lina changamoto zake, lakini pia ilikuwa uzoefu mzuri na kipindi kizuri kwangu kama kocha.”
Ramovic amekiri, Algeria kila mchezo ni lazima ushinde na hakuna nafasi ya kufanya makosa.
“Belouizdad ni tofauti kabisa. Hapa lazima ushinde. Usiposhinda, lawama zinakuja mara moja: kocha si mzuri, wachezaji si wazuri, mabadiliko yafanyike. Huo ndio uhalisia,” amesema Ramovic na kuongeza;
“Algeria, kocha anaweza kukaa miezi mitatu au minne tu. Mimi nimekaa mwaka mmoja sasa, jambo ambalo tayari linanifanya kuwa miongoni mwa makocha waliodumu muda mrefu zaidi hapa. Lakini lengo si kudumu, lengo ni kushinda.”
Ramovic ana matumaini ya kuleta mafanikio msimu huu, ingawa timu yake ipo nafasi ya pili kwa mbali nyuma ya MC Alger inayofundishwa na Rhulani Mokwena, kocha ambaye walikuwa na uhusiano mbaya walipokutana kwenye PSL.
CR Belouizdad ipo nyuma kwa pointi 12.
Itakutana na MC Alger katika mechi ya robo fainali ya Kombe la Algeria mnamo Machi 3, mechi ambao unaweza kuwa muhimu sana kwa Ramovic.
Hata hivyo, Belouizdad inaongoza Kundi C la Kombe la Shirikisho ikifikisha pointi tisa baada ya jioni ya leo dhidi ya Stellenbosch kwa mabao 3-0 ikiwa ni mechi ya raundi ya nne.
Kundi hilo lina Otoho d’Oyo ya Congo ilishinda jioni hii ikiwa nyumbani kwa mabao 2-1 dhidi ya Singida Black Stars ya Tanzania inayoburuza mkia ikiwa na pointi nne kama Wasauzi.
“Bado tupo robo fainali ya kombe na tupo nafasi ya pili katika Ligi. Hiyo inaonyesha matarajio ni makubwa,” amesema Ramovic na kuongeza;
“Lazima tushinde kitu. Tusiposhinda, mimi nitabadilishwa na baadhi ya wachezaji pia watabadilishwa. Hiyo ndio presha, lakini ndio changamoto. Hiki ndicho kiwango ambacho unaweza kushinda vikombe na ndio maana niko hapa.”
Kocha huyo pia alionyesha furaha yake kurudi Afrika Kusini, akionekana siku zote alipenda maisha yake ndani ya PSL.
“Ni hisia nzuri sana kurudi katika nchi hii nzuri,” amesema mapema leo kabla ya mechi ya Cape Town. “Nilikaa hapa karibu miaka mitatu na nilikutana na watu wengi wazuri, hivyo kurudi kunanifanya niwe na furaha na fahari. Daima ni furaha kuwa hapa,” amesema Ramovic.
Akiwa Yanga Ramovic aliyechukua nafasi ya Miguel Gamondi aliyetimuliwa baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu Bara msimu uliopita aliiongoza timu hiyo kwa siku 81 katika mechi 13, akishinda tisa, kutoka sare mbili na kupoteza mbili zote zikiwa za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Rekodi ya Ramovic akiwa na Yanga Bara
LIGI KUU BARA
Ushindi: 6
Kupoteza: 0
Mabao ya kufunga: 22
Mabao ya kufungwa: 2
KOMBE LA SHIRIKISHO (FA)
Ushindi: 1
Kupoteza: 0
Mabao ya kufunga: 5
Mabao ya kufungwa: 0
LIGI YA MABINGWA AFRIKA
Ushindi: 2
Kupoteza: 2
Mabao ya kufunga: 5
Mabao ya kufungwa: 6