
Idsra ya Ujasusi ya Somalia (NISA) inasema kuwa Jumapili ilifanya operesheni dhidi ya kundi la kigaidi lenye uhusiano na Al Qaeda la Al Shabaab, na kuwaua wanachama wake 13, ikiwemo viongozi wake watano.
Operesheni hiyo ilifanyika katika eneo la Maha Saed katikati mwa Shabelle, ikilenga mkutano wa viongozi wa Al Shabaab.
“Viongozi hawa makatili waliolengwa walikuwa wanafanya mkutano wa kupanga njama ya mashambulizi ya kigaidi na kuweka shinikizo kwa jamii kuwaunga mkono. Hata hivyo, maafisa wa kijasusi walifanikiwa kuzima njama zao baada ya kukabilia wakiwa kwenye kikao chao,” NISA ilisema kwenye taarifa.
Shirika hilo liliwataja viongozi hao waliouawa kuwa ni Moalim Aseyr, Moalim Muhumed Ahmed Hassan, Sheikh Ali Guuraale, Abdirahman Sheikh Ali Dhegey, na Moalim Adey.
Operesheni mahsusi
Inasema kuwa walikuwa wanahusika na mashambulizi ya kigaidi yaliyofanyika katika eneo la katikati mwa Shabelle, Galgaduud, na Bay.