1.Kivuko cha Rafah chafunguliwa rasmi
Jarida letu hii leo la mwanzo wa wiki linaanza na habari njema huko Mashariki ya Kati ambako kivuko cha Rafah, ambacho ni mpaka wa Misri na na Ukanda wa Gaza eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu na Israel kimefunguliwa rasmi hii leo na kitaruhusu pamoja na mambo mengine wagonjwa kutoka kwenda kupata matibabu yanayohitajika na misaada kuingia kwa urahisi katika Ukanda wa Gaza.
Washiriki wa jumuiya katika tamasha la ndani linaloungwa mkono na UNMISS nchini Sudan Kusini, wakisherehekea amani na biashara kupitia sanaa za kitamaduni.
2. Sudan Kusini iko nijia panda na wananchi wanalitambua hilo: UNMISS
Sudan Kusini iko katika njia panda na wakati muhimu sana baada ya miaka ya migogoro, taifa changa zaidi duniani linakabiliwa na chaguo gumu, kurejea katika vurugu kubwa za maafa, au kusonga mbele kuelekea amani. Mpango wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo UNMISS unasema wananchi wana sauti ya kudhihirisha mwelekeo.
Mjini Mangalla wakati viongozi wa kisiasa wakiendelea kugawanyika, katika mji huu mdogo wa jimbo la Equatoria ya Kati, wananchi wa kawaida wanachagua njia tofauti. Hapa, familia kutoka pembe zote za nchi wanaishi pamoja. Zaidi ya makabila sitini na nne huita Mangalla nyumbani. Licha ya hofu, ugumu wa maisha na hali ya kutokuwa na uhakika, wakazi wanaamua kuzungumza badala ya kupigana.
Katika mazungumzo hayo ya kijamii yanayoungwa mkono na UNMISS, wanawake wako mstari wa mbele kuhimiza amani. Najwa Suleiman kiongozi wa wanawake ni miongoni mwao anasema, “tujiepushe na siasa. Tukianza kusikiliza wanaume na kutenda maneno yao, tutaiharibu nchi yetu. Sisi wanawake hatuna tatizo lolote kati yetu. Tatizo liko kwa wanaume wanaosambaza kauli za chuki miongoni mwa watu.”
Wanufaika wa mradi wa umwagiliaji mkoani Dodoma nchini Tanzania wakikagua mifereji ya umwagiliaji. Mradi hu umefanikishwa na Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya Mitaji UNCDF kwa ushirikiano na wadau wake ikiwemo serikali ya Tanzania.
3. UNCDF: Uwekezaji bunifu wasaidia wakulima Dodoma, Tanzania
Ukame ulipokumba Kijiji cha Kitati mkoani Dodoma mji mkuu wa Tanzania, Hadija Hussein mwenye umri wa miaka 70 alilazimika kuuza mifugo yake yote ili aweze kuishi. Kama wakulima wengine, hivi sasa amegubikwa na hofu kuwa pengine ukame kama huo unaweza kuibuka tena, lakini ndipo Umoja wa Mataifa ukachukua hatua kuondoa hofu hiyo.
Bi. Hadija Hussein akiwa ameketi nyumbani kwake akikumbuka ukame uliomlazimu kuuza mali zake anasema nilijihisi vibaya sana katika hali ile, nilisalia bila kufahamu la kufanya.
Hofu yake hiyo ilipatiwa jawabu na Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya Mitaji, UNCDF, ambao unasaidia wanaokumbwa na madhara ya mabadiliko ya tabianchi kujijenga mnepo ili changamoto hizo zinapotokea waweze kuhimili na kuendelea na maisha.
Video ya UNCDF inatupitisha kwenye shamba moja hapa Kitati wilayani Mpwapwa, moja ya wilaya za mkoa wa Dodoma, kwa uwezeshaji wa UNCDF miundombinu ya umwagiliaji ikiwa imejengwa na mifereji iko bayana kuelekeza maji kwenye mashamba.
Bofya hapo chini kusikiliza taarifa nzima.