Akiwa mjini Moscow, msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alisema awali mkutano huo ulikuwa umepangwa kufanyika Jumapili. Haya ni kulingana na Interfax. Hata hivyo Peskov ameongeza kuwa mipangilio zaidi ya wajumbe wa pande hizo tatu ilikuwa muhimu.
”Ni mchakato mgumu wenye mwelekeo mbalimbali. Katika baadhi ya masuala, kwa hakika tumepiga hatua kwasababu kumekuwa na majadiliano, mazungumzo, na katika baadhi ya masuala ni rahisi kupata muafaka. Kuna masuala ambayo ni vigumu zaidi kupata muafaka, kwa bahati mbaya, bado hakuna makubaliano.”
Peskov ameripotiwa akisema duru ya pili sasa itafanyika Jumatano na Alhamisi huko Abu Dhabi.
Tarahe hizo zinalingana na zilizotolewa na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky siku ya Jumapili.
Watu wawili wauawa katika shambulizi la Urusi Donetsk
Shambulizi la Urusi katika mji wa kiviwanda wa Oleksievo-Druzhkivka kwenye eneo pana la Donetsk, limewauawa mwanamume wa umri wa miaka 44 na mwanawe wa umri wa miaka 23. Haya yameripotiwa na polisi huku mama wa familia hiyo na watoto wengine wawili wakijeruhiwa.
Polisi inasema mwezi Novemba mwaka jana, familia hiyo ilikimbia eneo la Donetsk, ambalo Kremlin inadai ni sehemu ya Urusi, lakini ikarejea mwezi mmoja baadaye.
Mamlaka za eneo hilo ambazo zimewataka wakaazi kuondoka katika maeneo ya mstari wa mbele wa vita, mara kwa mara huripoti kuhusu wakimbizi wanaorejea na kisha kuuawa.
Mwanadiplomasia wa Urusi afukuzwa Uingereza
Uingereza imesema leo kuwa imemfukuza mwanadiplomasia mmoja wa Urusi baada ya kumuita balozi wa nchi hiyo katika kile ilichosema ni hatua ya kisasi baada ya mwezi uliopita Moscowkumfukza mwanadiplomasia wa Uingereza, na kumshtumu kwa kuwa afisa wa ujasusi asiyejulikana.
Katika taarifa leo, msemaji wa ofisi ya mambo ya nje ya Uingereza FCDO amesema shtuma za Urusi hazikuwa na msingi na kufukuzwa kwa mwanadiplomasia huyo haikuwa haki.
Afisa mmoja mwandamizi wa FCDO aliweka wazi kwamba Uingereza haitavumilia vitisho kwa wafanyakazi wa ubalozi wake.
Ubalozi wa Urusi mjini London haukujibu haraka ombi la tamko kuhusiana na hali hiyo.
Ujerumani yawazuia watu watano kwa kusafirisha bidhaa Urusi
Ujerumani imewazuia watu watano mjini Luebeck kaskazini mwa nchi hiyo na wilaya ya Herzogtum Lauenburg wanaoshukiwa kuendesha mtandao unaosafirisha nje bidhaa kwa kampuni za ulinzi za Urusi na kukiuka vikwazo vya Umoja wa Ulaya vilivyowekwa baada ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Haya yamesemwa leo na waendesha mashtaka wa taifa hilo la shirikisho.
Ubalozi wa Urusi mjini Berlin haukujibu mara moja ombi la tamko kuhusu mashitaka hayo.