Johor Bahru iko mwisho wa Malaysia wa mpaka wa kilomita moja kuelekea Singapore na ni maarufu miongoni mwa wanunuzi wa bajeti.

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Mariam Mjahid
    • Nafasi, Mwandishi BBC Swahili
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Kwa miongo kadhaa, viongozi wa Kenya wamekuwa wakitamani kuigeuza nchi hii iwe kile walichokiita “Singapore ya Afrika.” Ni ndoto iliyovaa sura nyingi, ikibadilisha maneno lakini ikibaki na kiini kile kile: hamu ya kutoka uchumi wa kipato cha kati unaoyumba, na kuingia ligi ya mataifa tajiri, yenye nidhamu, ufanisi na taasisi imara.

Rais William Ruto ameifufua ndoto hiyo kwa ari kubwa. Kwa kauli zake, Kenya haitaki tena kusonga taratibu; anataka “kuinyanyua” nchi iingie haraka katika kundi la uchumi wa kipato cha juu.

Lakini hii si ndoto mpya wala si ya kipekee kwake wala mtangulizi wake Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.

Msururu wa kidiplomasia kutoka kwenye mkutano huo zinaonyesha maafisa wa Marekani wakipendekeza kongamano la sera ya idadi ya watu jijini Nairobi “kuchochea maslahi katika tatizo,” wazo ambalo Moi na wasaidizi wake walikaribisha.

Miongo minne baadaye, nia hiyo inadumu, lakini safari inabaki bila ramani.

Matarajio ya Kenya ya Singapore yanaendelea kuenea ikiwa ni lugha inayopendwa na wanasiasa wanapopanda majukwaani na umma haswa vijana mitandaoni kuuona kama udanganyifu wa muda mrefu wa kitaifa.

Uhuru Kenyatta pia alitania kwa kulinganisha Kenya na Singapore.

Katika ziara ya mwaka wa 2019 nchini Singapore alisifu jimbo la jiji kama kielelezo cha Dira ya Kenya ya 2030.

Rais Ruto, ambaye mara kwa mara anataja nidhamu na ufanisi wa Singapore, bado hajazuru nchi hiyo.

Historia ya Kenya kujilinganisha na Singapore

Mwaka 1980, Rais Daniel arap Moi alipokuwa Ikulu ya White House, Rais Jimmy Carter alimkabili kwa wasiwasi usiotarajiwa: ongezeko la kasi la idadi ya watu nchini Kenya.

Carter alihoji ikiwa Moi “baba wa watoto saba” angeweza kwa uhalisia kuongoza kampeni ya kitaifa ya uzazi wa mpango.

Moi alijibu kwa kumrejelea Singapore.

Alisema alikuwa akisoma kwa makini nidhamu ya kidemografia na mfano wa maendeleo wa nchi hiyo ndogo ya Asia, akitamani kuubadilisha na kuutumia Kenya. Carter alikubali kwamba Lee Kuan Yew alikuwa amefanya “kazi nzuri,” lakini akaweka tahadhari muhimu: Singapore ni ndogo; Kenya si ndogo.

Miaka arobaini baadaye, ndoto bado ipo lakini ramani ya kufika huko bado haijaandikwa.

Kwa nini Singapore? Kuna nini huko?

Singapore si hadithi ya miujiza.

Ni hadithi ya dola yenye uwezo mkubwa.

Waziri mkuu mwanzilishi wa Singapore, Lee Kuan Yew, alijijengea urithi ambao sasa unasifiwa kote barani Afrika hasa nchini Kenya na Rwanda, nchi mbili zinazopenda kutumia mbinu zake.

Lee Kuan Yew alijenga taifa juu ya misingi mitatu isiyoyumba:

  • Mamlaka yenye ufanisi na nidhamu ya juu
  • Mwendelezo wa taasisi, si watu
  • Uhamisho wa madaraka ulio safi na uliopangwa

Zote tatu kenya imekuwa na changamoto nazo.

Warithi wake, ikiwa ni pamoja na Waziri Mkuu wa sasa Lawrence Wong, wanaendesha serikali kama kampuni inayopima matokeo: mawaziri walichaguliwa kwa uwezo wa kitaaluma, walilipwa mishahara ya juu ili kuua tamaa ya rushwa, na walipimwa kwa viashiria vinavyoonekana.

Singapore iliua rushwa mapema na bila msamaha.

Ofisi ya Uchunguzi wa Rushwa (CPIB) inaripoti moja kwa moja kwa waziri mkuu, na inaichukulia rushwa kwa uzito ambao mataifa mengine hutumia kwa ‘kesi za ugaidi’.

Kashfa moja tu, kiongozi wa Singapore anaondolewa madarakani. Hakuna “kurudi serikalini kupitia mlango wa nyuma.”

Kenya, kwa upande mwingine?

Wachambuzi wa siasa wanasema mara nyingi kashfa ndiyo mwanzo wa kupandishwa cheo.

Zaidi ya hapo, Singapore hupanga maendeleo kwa miaka 30 huku Kenya hupanga kwa mzunguko wa uchaguzi wa miaka 5.

Singapore imeorodheshwa na shirika la Transparency ya 5 duniani kwa utawala safi

Kenya iko mbali kabisa.

Kenya iko wapi kwenye mlinganisho huu?

Kenya, kinyume chake, imekuwa ikijaribu kila kitu lakini kwa wakati mmoja. Ina nishati, ubunifu, na rasilimali watu.

Ruwaza ya ‘Vision 2030’, iliyozinduliwa kwa mbwembwe, sasa iko karibu kufikia tarehe yake ya mwisho huku ikionekana zaidi kama kauli mbiu iliyochoka kuliko mpango uliokamilika.

Rais Ruto anataka nini haswa?

g

Chanzo cha picha, Bloomberg via Getty Images

Rais wa Kenya William Ruto anasisitiza kuwa serikali yake inaweka misingi ya kuibadilisha Kenya kuwa “Singapore ya Afrika,” akisema kuwa mageuzi yatazaa matunda “mapema zaidi kuliko wakosoaji wanavyofikiria.”

Wafuasi wake wanaona serikali ikifanya kazi kupitia msuguano huo; wakosoaji wake wanaona serikali inaiunda.

Rais Ruto ameonekana kubadilisha dira yake ya kuwarubuni wapiga kura hasa ikiwa imesalia mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu.

Ikumbukwe mwaka 2022 Ruto aliingia madarakani kwa kauli ya kuwarahisishia maisha wananchi wa kipato cha chini almaarufu ‘hasla’. Kauli ambayo iliaminiwa na wengi na wimbi lake lilimuingiza katika ikulu.

Miaka mitatu baadaye Ruto amebadilisha alichokiamini hapo nyuma na sasa kuahidi wananchi kuwa atawapeleka Singapore yaani ataigeuza nchi iwe katika hadhi ya juu na itawarahisishia riziki wengi.

Kwanza kabisa aliahidi kuanzisha mpango wa KSh trilioni 5 wa Mfuko wa Kitaifa wa Miundombinu na unakusudia:

  • kujenga barabara kuu 2,500 km,
  • kukarabati barabara 28,000 km,
  • kupanua reli ya SGR hadi Malaba,
  • na kuzalisha megawati 10,000 za umeme.

Itatuchukua muda gani kufika Singapore?

Ratiba za safari kutoka hadhi ya ulimwengu wa kwanza hadi Singapore, Malaysia, Hong Kong na nchi zingine za ulimwengu wa kwanza zimepitia mabadiliko makubwa kulingana na wakati.

Takriban mwezi mmoja uliopita, alipowasilisha mradi wake kabambe wa Ksh.5 trilioni kwa Bunge wakati wa Hotuba yake kwa Taifa, Rais Ruto aligusia dira yake kwa mara nyingine tena, akitangaza kwamba nguzo 4 zinazoimarisha mpango wake wa uwezeshaji kiuchumi zingechukua miaka 10 kutekelezwa.

Walakini, miezi miwili mapema, safari hiyo ilikuwa ndefu zaidi ya miaka 10.

“Tunataka kuhamisha nchi hii kutoka nchi ya ulimwengu wa tatu hadi nchi ya ulimwengu wa kwanza katika miaka 30 ijayo, ambayo ni ifikapo 2055,” alisema Oktoba 12, 2025.

Rais pia amerekebisha nguzo muhimu zinazoimarisha mpango wake kutoka 4 hadi tatu alipohutubia taifa wakati wa Siku ya 62 ya Jamhuri.

Ndani ya miezi michache, ratiba ya “safari ya Singapore” imebadilishwa mara tatu: miaka 30, kisha 10, sasa “nusu tayari ifikapo mwaka ujao.”

”Hii si lugha ya mipango ya muda mrefu, ni lugha ya siasa”, wachanganuzi wa siasa nchinihumo wameendelea kuchambua lugha inayotumika na kiongozi huyo ameweka nia ya kuingoza Kenya kwa muhula wa pili wa miaka mitano.

Ndoto inayowezekana au siasa?

Kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, ambaye pia ni upande wa upinzani nchini Kenya ameikosoa vikali ndoto hii, akiita kulinganisha Kenya na Singapore kuwa aibu ya kidiplomasia.

Alipendekeza kuwa badala yake Kenya inafaa kubuni mifumo ya maendeleo ya watu wa nyumbani sawa na Dira ya 2030, ambayo ilizinduliwa wakati wa Serikali ya Muungano Mkuu ambapo alihudumu kama Makamu wa Rais.

“Unafanya kile ambacho Kibaki na sisi tulifanya, Dira ya 2030,” Kalonzo alikariri.

Kiongozi wa Wiper aliangazia mifumo ya upangaji ya muda mrefu ya bara na ya kitaifa kama mbinu mwafaka zaidi za maendeleo endelevu.

Makamu wa Rais wa zamani Kalonzo Musyoka amepuuzilia mbali ulinganisho wa Singapore kama mpango mwingine wa serikali ambao haukufanikiwa, akiufananisha na Mfuko wa ‘Hustler’, ambao umekabiliwa na ukosoaji juu ya utekelezaji na athari zake.

Miaka 40 imepita, Kenya bado iko njiani, bila ramani iliyo wazi.

Kwa sasa, ulinganisho huo bado ni wa kutamaniwa tu. Singapore ni dola yenye uwezo mkubwa, siasa zenye nidhamu, urasimu wa wasomi, na kutovumilia rushwa.

Imehaririwa na Ambia Hirsi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *