
Mpatanishi mkuu wa Ukraine Rustem Umerov ameyaeleza mazungumzo yaliyofanywa upya huko Abu Dhabi kuhusu kufikisha mwisho vita vya Urusi dhidi ya Ukraine kama yenye maana na tija, akisema yalilenga hatua maalum na suluhisho la vitendo.
Mazungumzo yanatarajiwa kuendelea leo Alhamisi, kwa mujibu wa vyombo kadhaa vya habari, vikilinukuu Baraza la Usalama na Ulinzi la Kitaifa la Ukraine.
Umerov alitaja uwezekano wa kubadilishana zaidi wafungwa kati ya Urusi na Ukraine, taarifa iliyoungwa mkono na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky katika hotuba yake ya video ya usiku.
Umerov alitangaza kwenye televisheni ya Ukraine kwamba ujumbe wa Kiev pia utajadili makubaliano kuhusu dhamana za usalama na ujenzi upya pamoja na Marekani.