Tangazo la kufanyika mazungumzo hayo limetolewa na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran Abbas Araghchi, saa kadhaa baada ya mashaka kwamba mazungumzo hayo huenda yasifanyike kutokana na mabadiliko ya muundo na maudhui yake.
Hapo jana Jumatano (04.05.2026), afisa mmoja wa Iran ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema nchi hiyo inataka kuwa na mazungumzo tofauti yanayohusiana na mpango wake wa nyuklia pekee na watakaoshiriki ni wajumbe tu wa nchi hizo mbili. Nae afisa wa Ikulu ya Marekani, White House ambaye pia hakutaka jina lake litajwe alisema viongozi kadhaa wa Kiislamu na wa Kiarabu walimrai Rais Donald Trump kutoyafuta mazungumzo hayo licha ya Iran kutoa masharti ya kitakachojadiliwa.
Marekani hata hivyo imethibitisha kuwepo katika mazungumzo ya kesho (06.05.2026), na kuwa na matumaini kwamba yatakwenda vizuri huku Waziri wa mambo ya nje wa taifa hilo Marco Rubio akisema anatumai majadiliano yatakuwa mapana na sio tu kujadili mpango huo wa nyuklia.
Iran Kwa miongo kadhaa imekuwa ikisisitiza kuwa mpango wake wa nyuklia ni wa amani, lakini maafisa wake katika miaka ya hivi karibuni wamekuwa wakitishia kutengeneza silaha za nyuklia na wamekuwa wakirutubisha madini ya urani kwa kiwango cha asilimia 60, ambacho kinakaribia asilimia 90 ya uwezo wa kutengeneza silaha hizo za nyuklia.
Trump atoa onyo kali kwa Ayatolla Ali Khamenei
Licha ya hayo, Rais Trump ametoa onyo kali kwa Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatolla Ali Khamenei kabla ya mazungumzo hayo kwamba anapaswa kuwa na wasiwasi mkubwa.
“Naweza kusema kwamba anapaswa kuwa na wasiwasi mno, ndio lazima awe na wasiwasi. Kama unavyojua Iran inajadiliana na sisi. Walikuwa wanafikiria kuwa na eneo jipya la nyuklia katika sehemu tofauti ya nchi, tuligundua hilo nikasema mukifanya hivyo basi tutawafanyia kitu kibaya zaidi,” alisema Trump.
Mvutano kati ya mataifa hayo mawili ulizidi kutanuka baada ya Trump kupendekeza kuwa Marekani inaweza kuiingilia kijeshi nchi hiyo, kutokana na madai ya kuwakamata na kuwaua waandamanaji walioipinga serikali. Maandamanao hayo yaliyofanyika mwezi uliopita kwa zaidi ya wiki mbili yanadaiwa kusababisha vifo vya zaidi ya Wairani 6,000 huku wengine 50,000 wakikamatwa hii ikiwa ni kwa mujibu wa wanaharakati wa kutetea haki za binaadamu wa Marekani.
Wakati huo huo, Iran pia imeikaripia Ujerumani siku moja baada ya Kansela wa taifa hilo Friedrich Merz, kusema ataiwekea Jamhuri hiyo ya Kiislamu vikwazo vipya, iwapo haitoacha vurugu dhidi ya raia wake na kuachana na mpango wake wa nyuklia. Iran imesema inasikitika kwamba Ujerumani inageuka kuwa mchokozi badala ya kuwa taifa linalopenda maendeleo barani Ulaya ikisema inatumai uongozi imara na thabiti utarejea Ujerumani.
Serikali ya Ujerumani imesema ipo katika mawasiliano mazuri na Uingereza, Ufaransa, Marekani na Israel na washirika wengine wa kikanda imesema amani na usalama wa kikanda ni suala muhimu kwa nchi hiyo.
