
Dar es Salaam. Wakati familia zinapokabiliwa na dharura za kiafya, jamii inapoandaa shughuli za misiba, au wazazi wanapojipanga kuandaa harusi ya mtoto wao, ukusanyaji wa michango huwa ni pasua kichwa. Ucheleweshaji na ukosefu wa uwazi. Kufuatilia nani alichanga, kiasi gani kimekusanywa na kutuma fedha kupitia mitandao tofauti mara nyingi huongeza changamoto katika kipindi ambacho tayari kina uzito.
Ili kurahisisha hali hii ambayo ni kawaida kwa Watanzania, kampuni ya huduma za kifedha kwa njia ya simu, Mixx, kwa kushirikiana na Benki ya Azania imezindua huduma ya Mchango, jukwaa jipya la kidijitali linalowezesha ukusanyaji, utumaji na usimamizi wa michango kwa urahisi, na uwazi.
Huduma hii inayopatikana kupitia Mixx Super App, Mchango inatatua changamoto mbalimbali za watanzania. Jukwaa hili linamwezesha mtumiaji kuratibu michango mahali pamoja huku likitoa mwonekano wa papo hapo kuhusu makusanyo na malipo.
Huduma ya Mchango ambayo inapatikana kwenye Super App ya Mixx, inalenga kuondoa changamoto zilizokuwa zikiwakabili wananchi katika uratibu wa michango-ikijumuisha ucheleweshaji wa taarifa, ugumu wa kufuatilia ahadi, pamoja na urasimu wa kutuma au kupokea michango kutoka kwenye mitandao mingine au huduma za kibenki.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huduma hiyo leo jijini Dar es Salaam, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mixx, Angelica Pesha, alisema huduma hiyo imebuniwa kwa kuzingatia uhalisia wa maisha ya Mtanzania na utamaduni wa kusaidiana katika matukio mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.
“Watanzania tumekuwa tukichangiana katika nyakati za huzuni kama misiba, matibabu na changamoto za kimaisha, lakini pia kwenye furaha kama harusi, send-offs, kitchen parties na shughuli mbalimbali za kimaendeleo.” alisema Pesha. “Kupitia Mchango, tunatambulisha huduma rahisi, salama na jumuishi inayowaunganisha watumiaji wa Mixx na nje ya Mixx sambamba na wateja wa benki kote nchini. Hii ndiyo taswira halisi ya ujumuishi wa kifedha.”
Kupitia Mchango, watumiaji wanaweza kuratibu michango ya harusi, ada za shule, vikundi vya uwezeshaji, miradi ya kijamii, kampeni za maendeleo na shughuli nyingine za kijamii- zote ndani ya jukwaa moja la kidigitali linalotoa uwazi na ufuatiliaji wa papo kwa hapo.
Pesha aliongeza kuwa uzinduzi wa huduma ya Mchango ni sehemu ya mkakati mpana wa Mixx katika kuendelea kuwekeza katika teknolojia, usalama na ubunifu ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma za kifedha zinazokidhi mahitaji ya sasa na yajayo.
“Leo ni mwanzo wa ukurasa mpya katika safari yetu ya kuboresha huduma za kifedha nchini. Tunaamini Mchango itaratibu michango kwa ufanisi zaidi, kuimarisha mshikamano wa kijamii na kurahisisha maisha ya watumiaji wetu kote nchini,” aliongeza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo huduma za Benki Kidigitali, Vinesh Davda, alisema ushirikiano huu unaonesha namna teknolojia na ubia vinavyoweza kufungua fursa za kifedha jumuishi.
“Teknolojia ina nafasi muhimu katika kufanya huduma za kifedha zipatikane kirahisi, bora na ziendane na mahitaji ya kila siku ya watu,” alisema. “Kupitia ushirikiano huu na Mixx kwenye Mchango, tunaunganisha nguvu kuunda suluhisho linalounga mkono mahitaji ya kifedha kwa jamii, huku huduma ikipatikana kupitia majukwaa ya benki na simu. Huu ndiyo aina ya ubia unaohitajika kuendeleza ujumuishi wa kifedha nchini.”
Mchango sasa inapatikana kwa watumiaji wote wa Mixx, pamoja na Watanzania wanaotumia huduma za benki na mitandao mingine ya kifedha, ikiwa njia rahisi na shirikishi zaidi ya kusaidiana pale panapohitajika.