Dar es Salaam. Ushindani wa Tyla, 24, katika tuzo za Grammy, kwa mara nyingine umegeuka mwiba kwa mashabiki wa tasnia ya muziki huko Nigeria hasa wale wa Davido, 33, ambao wanalalamika wakidai alistahili ushindi.
Hata hivyo, Tyla kutokea Afrika Kusini, hana namna zaidi ya kuendelea kufanya kile anachofanya mara zote, na kwa muktadha huo, mashabiki wa Davido na wa washindani wengine wajiandae kulia zaidi!.
Katika tuzo za 68 za Grammy 2026 zilizotolewa wikiendi iliyopita huko Los Angeles, Marekani, Tyla alishinda kipengele cha ‘Best African Music Performance’, ambacho ni maalumu kwa muziki wa Afrika.
Ushindi huo wa Tyla umekuja kupitia wimbo wake, Push 2 Start (2024), ambao umewazidi kete washindani wake; Burna Boy (Love), Davido (With You), Eddy Kenzo (Hope & Love) na Ayra Starr (Gimme Dat).
Hii inakuwa mara ya pili kwa Tyla kushinda kipengele hicho kilichotambulishwa na waandaaji wa tuzo hizo, Recording Academy kwa mara ya kwanza hapo Juni 2023, na kuanza kutumika msimu wa 2024.
Lakini kwa nini mashabiki wengi wa Davido wanalalamikia ushindi wa sasa wa Tyla? Ingawa zinatajwa hoja nyingi ambazo baadhi zinakosa uthibitisho kabisa, ila kuna moja naweza kuizungumzia.
Katika kiwanda cha muziki Nigeria kuna kile wanachoita ‘Big Three’ wakimaanisha wasanii wakubwa watatu ambao ndio hasa wenye ushawishi mkubwa na ndio wanaoibeba tasnia hiyo kwa wakati huo.
Utatu huo unaundwa na Burna Boy, Wizkid na Davido mwenyewe, lakini baadhi ya wasanii wengine akiwamo Tiwa Savage, wamekuwa wakipinga hilo wakisema muziki wa Nigeria ni zaidi ya watatu hao.
Sasa katika hawa watatu, ni Davido peke yake ndiye hajashinda tuzo ya Grammy, na hii mara zote imetumika na mashabiki wa washindani wake kama fimbo ya kumchapia wakidai hastahili kuwamo katika ‘Big Three’.
Na hilo hasa ndio limekuwa likiwapa hasira mashabiki wa Davido, wao wanaona anastahili kushinda Grammy bila kujali kama ana kazi nzuri, bali wanachohitaji ni kutimiza matakwa yao ya kiushindani katika soko la Nigeria.
Tunapata picha ya msukumo wa agenda hii, kwa jinsi mashabiki hao wenye hasira walivyogeuka na kuanza kuwashambulia wasanii wengine wa ‘Big Three’ baada ya Davido kuikosa tena Grammy hapo juzi.
Wanabeza ushindi wa Wizkid katika Grammy 2021 wakisema kama asingeshirikishwa na Beyonce katika wimbo, Brown Skin Girl (2019) ambao ndio ulioshinda, basi hadi leo naye angekuwa hana Grammy!
Kwa Burna Boy, anasema ushindi wake wa Grammy 2021 kupitia albamu yake, Twice As Tall (202), umechangiwa na Diddy ambaye ndiye mtayarishaji wake mkuu, kwa hiyo, bila hivyo asingeambulia kitu.
Davido anajua yote hayo na ndio sababu amekuwa akionyesha wazi kuwa anahitaji kushinda Grammy na hata amehudhuria hafla zote, lakini kwa bahati mbaya mara zote mbili (2024 & 2026) ameangukia pua mbele ya Tyla.
Utakumbuka msimu wa 2024, Tyla alishinda kupitia wimbo wake, Water (2023), akiwabwaga wakali kama Asake (Amapiano), Burna Boy (City Boys), Davido (Unavailable) na Ayra Starr (Rush).
Hapa pia mashabiki wa Davido walilalamika, mmoja wapo ni mtangazaji Adesope Shopsydoo aliyewatupia lawama waandaaji wa Grammy akidai wamemtumia msanii huyo kutangaza tukio lao kisha wakamtosa.
Msimu uliopita ambapo Tems kutokea Nigeria alishinda kama ‘Best African Music Performance’ kupitia wimbo wake, Love Me Jeje (2024), kelele zote hizi hazikuwapo kwa sababu Tyla na Davido hawakuwania.
Staa wa muziki kutokea Kenya, Victoria Kimani, amekosoa vikali tabia ya baadhi ya mashabiki wa Nigeria kuamini wao ndio wanastahili kila kitu kizuri kilichopo katika soko la muziki Afrika.
“Tyla na timu yake wamevunja kuta ambazo Waafrika wengine wamekuwa wakiziweka dhidi ya Waafrika wenzao wanaoonekana na kusikika tofauti, au wasiokuwa wakiimba kwa lahaja yoyote ya Kiafrika.
“Mfano ni Waafrika kama mimi ambao tumekuwa tukichanganya muziki wa Kiafrika na Pop pamoja na R&B (AfroPop) kwa zaidi ya muongo mmoja, huku nikiwa nimetoa albamu tano hadi sasa.
“Upinzani anaoupata Tyla kwa ushindi wake huko Grammy, ni uleule ninaoupata kila ninapotoa kazi mpya; Watu huniambia, ‘Imba kwa Kiswahili’, ‘Hii haisikiki kama ya Kikenya’, n.k..
“Hatimaye, tuna mtu mmoja [Tyla] aliyewapita nyote kimawazo. Na nimeipenda hali hii… Pia ninyi hupenda kuchagua ni lini muwe ‘Waafrika’ huku mkiabudu kila kitu cha kigeni. Haya sasa, nyamazeni!” ameeleza Victoria Kimani.
Wakati mashabiki wa Davido wakiendelea kulalamika, kuna uwezekano mkubwa Tyla akashinda Grammy 2027. Awamu hii ni kupitia wimbo wake, Chanel (2025) ambao video yake imetazamwa YouTube mara milioni 83 ndani ya miezi mitatu tu!
Wimbo huo ambao ni wa kwanza kuachiwa kutoka katika albamu yake ijayo, A-Pop (2026), unatikisa sasa katika chati mbalimbali kubwa duniani ikiwamo Billboard Us Afrobeats Songs ambapo unashika namba moja.
Kumbuka nyimbo zote ambazo zimempa ushindi Grammy zilishika namba moja katika chati hiyo, na ndio sababu mashabiki wa Davido wanaambiwa msimu ujao kazi pia wanayo, kama ni kulia na kulalamika waanze sasa!