Dar es Salaam, Tasnia ya Bongo Fleva imejaa vipaji vingi vya kike vilivyoacha alama kubwa licha ya kudumu kwa muda mfupi. Cha kusikitisha ni kwamba baadhi ya wasanii hao walilazimika kuacha muziki wakiwa bado wanahitajika na tasnia, mashabiki pamoja na soko lenyewe la muziki.

Sababu za kuacha kwao zinatofautiana kuanzia changamoto za kisaikolojia, kifamilia, kiuchumi hadi wengine kiimani.

Mwananchi imekuletea baadhi ya wasanii wa kike waliouacha muziki wakati walipokuwa bado na nafasi kubwa ya kufanya makubwa zaidi.

BONG 03

1. Vanessa Mdee

Vanessa a.k.a Vee-Money ni mmoja wa wasanii wa kike waliofanya vyema kimataifa na kutabiriwa kuwa angaleta mapinduzi kwenye muziki wa Bongo Fleva.

Safari yake ilianza baada tu ya kushiriki Tusker Project Fame 2011, mwaka uliofuata alianza safari yake ya muziki, kabla ya kuachia wimbo wake mkubwa ‘Closer’ mwaka 2013 uliompa umaarufu.

Mwaka huohuo alisainiwa na lebo ya B’Hits ambayo kwa sasa inajulikana Bxtra Records na ndipo sasa akatambuliwa zaidi kama msanii wa kike kwani awali alikuwa akifanya shughuli za utangazaji.

Aliendelea kung’ara, akatoa albamu Money Mondays (2018) na kufanya kazi na lebo ya Universal Music Group (UMG) na baadaye kuanzisha lebo yake mwenyewe, Mdee Music.

Ngoma kama Kisela (2017) aliyomshirikisha Mr P mmoja wa wanachama la kundi la muziki la P Square nchini Nigeria, Move (2017) ft Reekado Banks, ‘Me and You’ na Ommy Dimpoz ni kati ya kolabo zilizompa umaarufu zaidi mwanadada huyo.

Hata hivyo, miaka miwili baadaye mkali huyo akatangaza rasmi kuwa ameachana na muziki ambao nyuma ya pazia ulikuwa na maumivu makubwa kwake.

Vanessa alisema muziki haukumlipa kwa kiwango kinacholingana na juhudi zake, alipata msongo mkubwa wa mawazo uliomfikisha karibu kupoteza maisha, aliingia kwenye ulevi uliokithiri na kujikuta akiishi maisha ya kuigiza kwa mashabiki.

Hivi sasa anaishi Marekani na mumewe na baba watoto wake wawili, muigizaji na mwimbaji, Rotimi.

BONG 04

2. Malaika

Malaika alikuwa miongoni mwa wasanii wa kike waliotabiriwa kuja kutawala Bongo Fleva. Alianza kwa kushirikishwa kwenye ‘Uswazi Take Away’ ya mkongwe Chegge (2014), lakini umaarufu wake ulianza kupitia wimbo ‘Rarua’ ambao ulipata wasikilizaji wakubwa Afrika Mashariki na remix ya Diamond Platnumz.

Nyimbo kama ‘Mwantumu’, ‘Sare’, ‘Nenda’ na ‘Zogo’ zilithibitisha kuwa alikuwa na sauti, mvuto na utambulisho wa kipekee. Zaidi ya hapo, alipata fursa ya kufanya kazi na mtayarishaji wa kimataifa David Roddie wa Urban Studios, Glasgow, Scotland.

Hata hivyo, licha ya fursa hizo, Malaika hakudumu kwenye ramani ya Bongo Fleva, sababu zake hazikuwekwa wazi hadharani, lakini ni wazi kuwa mfumo wa tasnia haukuwa rafiki kwake.

BONG 01

3. Recho Kizunguzungu

Recho ni zao la Taasisi ya THT na alionyesha mapema kuwa ana uwezo mkubwa wa kuwakilisha kizazi kipya cha wasanii wa kike. Alikuwa ujasiri na mtazamo tofauti.

Kipaji chake kiligunduliwa na mkurugenzi wa zamani wa THT, marehemu Ruge Mutahaba ambaye aliamini uwezo wa mwanadada huyo kwenye kuimba zaidi ya kuigiza.

Wimbo wa kwanza uliompa umaarufu mkubwa Recho ‘Kizunguzungu’ aliouachia mwaka 2011 alipoanza kupata mashabiki na hadi kupachikwa jina la Recho Kizunguzungu.

Aliendelea kutoa ngoma kama Upepo (2012), Nashukuru Umerudi (2013) zilizoendelea kumpa umaarufu, lakini ni kama nyota yake ilififia badala ya kuendelea kung’ara.

Ingawa hakutangaza rasmi kuondoka kwenye gemu, lakini ni muda mrefu hayuko kwenye ushindani na hata akitoa wimbo kuna baadhi ya mashabiki hawajui kama ameachia kibao, mara ya mwisho kuachia kazi ilikuwa 2024 ‘Saizi Yangu’ aliomshirikisha rapa Stamina.

BONG 05

Kwa watoto wa buku mbili wanaweza wasimfahamu kwa ukubwa mwanadada huyo, lakini wakati huo ndio alikuwa Shakira wa Bongo kutokana na ubunifu wa kutumia sauti na namna ya kuwaburudisha watu kupitia ‘Kiuno Bila ya Mfupa’.

Rehema Chalamila maarufu Ray C ambaye alianza sanaa yake mwanzoni mwa 2001 alivuma na nyimbo kama ‘Mapenzi Yangu’, ‘Sogea Sogea’, ‘Unanimaliza’, ‘Wanifuatia Nini’ na kutawala RnB ya Kiswahili.

Aliachia albamu nne ikiweamo Mapenzi Yangu (2003), Na Wewe Milele (2004), Sogea Sogea (2006), Touch Me (2008) na kunyakua tuzo mbalimbali ikiwamo TMA kama msanii bora wa kike mwaka 2004, Kisima Music Awards kama msanii bora wa kike kutoka Uganda na Tanzania na nyinginezo.

Baada ya kuugua na kurejea taratibu, Ray C hakuwahi kurudi kwenye ushindani wa juu kama awali. Ingawa bado mchango wake na alichokifanya kwenye muziki wa Bongofleva kinaheshimika.

BONG 02

Kwa sasa yuko bize zaidi na kuimba nyimbo za Injili ingawa hajatangaza rasmi kuacha Bongo Fleva, mara ya mwisho kuachia kazi ilikuwa mwaka jana alipotoa wimbo wa Leo akimshirikisha mzazi mwenzie Kusah.

Tangu hapo hajaonekana kwenye majukwaa yoyote ya muziki ingawa kwenye baadhi ya mahojiano aliyowahi kufanya alisema ameacha kwa sasa kuimba na anamtumikia Mungu.

Ni miongoni mwa wasanii zao la THT ambalo lilikuja na ushindani mkubwa kwenye muziki wa Bongofleva na wa kitofauti kutokana na sauti yake na kipaji alichokuwa nacho. ‘Jela’, ‘Ntade’ ni kati ya vibao vilivyofanya vizuri.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *